Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya leo tarehe 21.05.2019 limewafikisha Mahakama ya Wilaya ya Mbarali watuhumiwa watatu kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wa miaka sita aitwaye ROSE JAPHET, Namba ya Kesi PI 08/2019 ambapo watuhumiwa watatu wamesomewa kosa la mauaji.
Watuhumiwa waliofikishwa Mahakamani ni:-
JAPHET YAHAYA NGUKU [37] Mkazi wa Msewe – Igurusi Wilaya ya Mbarali [Baba Mzazi wa Marehemu].
ANDREW ANGANILE MWAMBULUMA [43] Mkazi wa Mapinduzi – Mbalizi [Mmiliki wa Shule ya Sekondari Ushindi].
MEJA JOTAM SANGA @ MESIA [48] Mkazi wa Ikonda Mkoa wa Njombe [Mganga wa Tiba Asilia].
Ni kwamba watuhumiwa mnamo tarehe 03.05.2019 majira ya saa 21:00 usiku huko Kijiji cha Msewe kilichopo Kata ya Igurusi, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya huko katika msitu wa hifadhi wa Chimala walimuua mtoto ROSE JAPHET kwa kumnyonga shingo na kisha kumkata kanyagio la mguu wa kushoto ambapo kanyagio la marehemu lilikutwa limefukiwa huko Mbalizi, Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Chanzo cha tukio hili ni tamaa ya kupata utajiri ambapo baba mzazi wa marehemu aitwaye JAPHET YAHAYA NGUKU alimtoa mwanae kwa ANDREW ANGANILE MWAMBULUMA ambaye ni mfanyabiashara kwa malipo ya Tshs 5,000,000/= ili auwawe na kisha kukatwa kanyagio la mguu wa kushoto na kupatiwa mfanyabiashara huyo ili apeleke kwa mganga ili amtengenezee ndagu (dawa ya utajiri) ili afanikiwe katika biashara zake za Shule anayoimiliki iitwayo Shule ya Sekondari Ushindi iliyopo Mbalizi.
Kesi ipo Mahakamani inangojea kutajwa tena tarehe 04/06/2019 Mahakama ya Wilaya ya Mbarali.
Imetolewa na:
[ULRICH O MATEI – SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.