Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisisitiza jambo kuhusu uzalendo na kuunga mkono Shirika la Mawasiliano TTCL jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………………………..
Na Paschal Dotto-MAELEZO-DAR ES SALAAM
RAIS Dkt. John Magufuli ameitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kutoa kipaumbele katika uwekezaji wa miundombinu ya mawasiliano kwa Kampuni ya Mawasiliano Nchini (TTCL) ili liweze kumiliki idadi kubwa ya minara ya mawasiliano ya simu na kumudu ushindani wa soko la mawasiliano nchini.
Akizungumza katika hafla ya upokeaji wa Gawio la Serikali la Tsh Bilioni 2.1 kutoka TTCL, leo Jumanne (Mei 21, 2019), Rais Magufuli alisema njia pekee ya kuiendeleza TTCL ni kwa Viongozi na Watendaji wa Serikali kuwa na moyo wa uzalendo wa kusimamia rasilamali za umma ikiwamo za shirika hilo.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema TTCL imekuwa ikitumia kiasi cha Tsh Milioni 700-800 kila mwezi kwa ajili ya kukodisha minara ya mawasiliano, wakati Serikali ina mfuko wa mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unaotoa ruzuku kwa makampuni mbalimbali ya mawasiliano kwa ajili ya kujiwekeza katika miundombinu ikiwemo minara ya mawasiliano maeneo mbalimbali nchini.
“Hili la TTCL kukopa minara katika makampuni mengine halikubaliki, Serikali ina mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) ambao wanatoa ruzuku kwa makampuni mengine ya simu lazima tulitazame upya, nataka sasa TTCL tuwape mitaji ya kutosha ili kuhakikisha kuwa linaendelea kupanua huduma zake kwa Watanzania wengi zaidi” alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inaipatia TTCL kiasi cha Tsh Bilioni 30 kilichobaki kati ya Tsh Bilioni 66 ilizotoa katika mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya kupanua mtandao wa huduma zake nchini, kwa kuwa Shirika hilo limeonesha mafanikio makubwa zaidi katika kipindi kifupi tangu serikali ichukue uamuzi wa kununua hisa zake kutoka kampuni ya Airtel mwaka 2016.
Akifafanua zaidi Rais Magufuli alisema Serikali itandelea kuiwezesha TTCL ili iweze kupanua mtandao wa mawasiliano yake nchini, na kuhakikisha kuwa linatekeleza vyema majukumu yake ikiwemo kusimamia mawasiliano ya Kimkakati nchini kupitia Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa kufuatia kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya TEHAMA mwaka 2016.