Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe ameweka wazi kwamba baada ya siku tisa Jengo la Tatu la abiria (TB III) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) litakabidhiwa rasmi kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) na kisha kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Waziri Kamwelwe amebainisha hayo leo alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo.
“Kwa ujumla mifumo mingi ya jengo hili imekamilika na kama kama mnavyoona sehemu nyingi zimeandikwa namba tisa (9) hiyo ina maana kwamba zimebaki siku tisa na kwa maana hiyo tarehe 29 Mei 2019 mkandarasi atakabidhi rasmi jengo”.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa TB III, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TANROADS Mhandisi Crispin Akoo alibainisha kwamba
kutokana maendeleo mazuri ya ujenzi Mkandarasi anatarajia kukabidhi jengo siku mbili kabla ya muda wa kwenye mkataba.
“Hadi kufikia terehe 31 Julai 2018 maendeleo yalikua ni asilimia 78.33 lakini hadi kufikia tarehe 18 Mei 2019 ujenzi wote ulikua umefikia asilimia 99.5”.
Kuhusu maandalizi ya uendeshaji Mkurugenzi Mkuu wa TAA Mhandisi Julius Ndyamukama alimweleza Waziri kwamba majaribio na maandalizi ya uendeshaji yalianza tangu mwezi machi mwaka 2018 na yapo katika hatua za mwisho.
“Majaribio ya kwanza ya kwanza ya mifumo na vifaa vinavyotumia umeme yalianza mwezi Julai 2018 kwa sasa yamefikia asilimia 96 na muda sio mrefu yatakamilika”.
Aidha Mhandisi Ndyamukama aliongeza kwamba majaribio hayo yanatarajiwa kufanyika ndani ya miezi mitatu kuanzia mwezi Mei na ifikapo mwezi Agosti yatakua yamekamilika.
Kwa ujumla mradi umeajiri wafanyakazi 1,179 ambapo asilimia 80 ni watanzania na asilimia 20 ni wafanyakazi wa kigeni.