Home Mchanganyiko PROFESA MBARAWA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA KIWANDA CHA MABOMBA

PROFESA MBARAWA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA KIWANDA CHA MABOMBA

0

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) akimsikiliza Meneja Biashara wa Kiwanda cha
Tanzania Steel Pipe (TSP), Ryan Koh (kushoto) alipofika kiwandani hapo.

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) akisisitiza jambo kwa Meneja Biashara wa Kiwanda cha
Tanzania Steel Pipe (TSP), Ryan Koh (kushoto) wakati wakiwa kwenye mazungumzo kiwandani hapo.

……………………

Waziri wa Maji, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (Mb) amefanya ziara ya kushtukiza kwenye Kiwanda cha Tanzania Steel Pipe (TSP) kilichopo Ubungo, jijini Dar es Salaam kinachojihusisha na utengenezaji wa mabomba baada ya kiwanda hicho kushindwa kupeleka mabomba kwenye miradi ya maji ya Nyang’hwale, Geita na Longido, Arusha kwa wakati.

Profesa Mbarawa amefika kiwandani hapo ili kufahamu tatizo linalosababisha mabomba hayo kushindwa kufika kwenye maeneo ya kazi “site” na kufanya utekelezaji wa miradi hiyo kusuasua bila sababu za msingi.
“Nimekuwa nikikerwa na tabia ya wakandarasi kushindwa kukamilisha miradi ya Nyang’hwale na Longido kwa sababu ya upatikanaji wa mabomba si mzuri bila kuwepo na sababu zozote za msingi”.

“Kufika kwangu kiwandani hapa ni kutaka kufahamu kuna tatizo gani kwa kuwa ndio wenye mkataba wa kupeleka mabomba kwenye miradi hiyo”, Profesa Mbarawa amesema.

Akiwa kiwandani hapo Profesa Mbarawa amekutana na Meneja Biashara wa TSP, Ryan Koh na kumpa onyo kuwa endapo wataendelea kutoheshimu mkataba huo na kuendelea kuwa sababu ya miradi hiyo kuchelewa hatasita kusitisha mkataba huo na kutafuta kampuni nyingine.

“Sitaweza kuvumilia hali hii wakati wananchi wanaendelea kuteseka, sitasita kuvunja mkataba na kutafuta kampuni nyingine hata kama ni ya nje ikibidi kwa sababu tumetoa fursa kwenu kampuni ya ndani lakini mnatuangusha”, Profesa Mbarawa ameonya.

“Nimeongea na Mkurugenzi wa Usambazaji wa Majisafi na Usafi wa Mazingira wizarani, ahakikishe kama kuna madeni yoyote mnayodai awalipe kufikia Jumatano. Nataka mpeleke bomba zote kwa wakati ili miradi hiyo iishe tuendelelee na maeneo mengine”, Profesa Mbarawa amesisitiza.

Aidha, Meneja Biashara wa TSP, Ryan Koh amesema amepokea ujumbe huo na wataanza kupeleka mabomba hayo mara moja katika maeneo ya kazi ya miradi hiyo na kumshukuru Profesa Mbarawa kwa kufika kiwandani kusikiliza changamoto zao.

Miradi ya Maji ya Nyang’hwale na Longido ni miongoni mwa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa na Serikali kwenye maeneo yenye changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa lengo la kufikisha huduma hiyo muhimu kwa kila mwananchi.