Home Mchanganyiko WABUNGE WAPITISHA KWA KISHINDO BAJETI YA WIZARA YA KILIMO

WABUNGE WAPITISHA KWA KISHINDO BAJETI YA WIZARA YA KILIMO

0

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) akitoa ufafanuzi wa hoja za wabunge zilizojitokeza kwenye Bajeti ya Matumizi ya kawaida ya wizara hiyo ya mwaka 2019/2020. Leo tarehe 20 Mei 2019 (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb) akionyesha ramani yenye ripoti ya afya ya Udongo wakati wa ufafanuzi wa hoja za wabunge zilizojitokeza kwenye Bajeti ya Matumizi ya kawaida ya wizara hiyo iliyosomwa kwa mwaka 2019/2020. Leo tarehe 20 Mei 2019

Sehemu ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakimpongeza waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb), Naibu maziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba na Mhe Innocent Bashungwa mara baada ya Bajeti ya Matumizi ya kawaida ya wizara hiyo kwa mwaka 2019/2020 kupita kwa kishindo, Leo tarehe 20 Mei 2019.

Sehemu ya wataalamu wa Wizara ya Kilimo wakiwa katika picha ya pamoja na waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb), Naibu maziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba na Mhe Innocent Bashungwa, Katibu Mkuu wa wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Prof Siza Tumbo mara baada ya Bajeti ya Matumizi ya kawaida ya wizara hiyo kwa mwaka 2019/2020 kupita kwa kishindo, Leo tarehe 20 Mei 2019.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo, Dodoma

Wabunge wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo tarehe 20 Mei 2019 wameridhia kwa kauli moja na kupitisha kiasi
cha Shilingi Bilioni 253.8 kwa ajili ya kugharamia matumizi ya kawaida na
miradi mbalimbali ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo kwa mwaka wa Fedha wa 2018/2019.


Wabunge hao wameridhia ombi la Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (Mb)
alilolitoa wakati akiwasilisha Bajeti ya Matumizi ya kawaida ya wizara hiyo
juzi tarehe 17 Mei 2019.

Akisoma
Bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Fedha za Wizara ya Kilimo kwa
Mwaka 2019/2020, Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga alisema, Serikali
imepanga kubadilisha kilimo kutoka kuwa cha kujikimu na kuwa kilimo cha
kibiashara kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Aidha, Mpango
wa Pili wa Taifa wa Maendeleo umesisitizia mapinduzi ya viwanda na umeitambua
Sekta ya Kilimo kuwa mhimili imara kwa ajili ya upatikanaji wa malighafi za
viwanda.  

Miongozo hiyo
ya Kitaifa, pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na Sera ya Kilimo
ya mwaka 2013, inatekelezwa na Wizara kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya
Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ambayo inalenga kuleta mageuzi katika Sekta ya
Kilimo na kwa kutambua umuhimu wa kuongeza mitaji, teknolojia na ubunifu, Sekta
Binafsi inashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa ASDP II.

Fedha nyingi
katika kiasi hicho cha Bilioni 253.8 zilizopitishwa na wabunge hao zitaelekezwa
kwenye utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)
iliyozinduliwa rasmi tarehe 4 Juni, 2018 na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inalenga kubadilisha
maisha ya mkulima kwa kufanya mageuzi makubwa kwenye kilimo kwa kuzingatia
mazao ya kipaumbele kulingana na ikolojia za kilimo.


Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa chakula katika mwaka 2018/2019 Waziri
Hasunga amesema upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2018/2019 ulifikia tani
milioni 16.89 zikiwemo tani milioni 9.53 za mazao ya nafaka na tani milioni
7.35 za mazao yasiyo nafaka. Kiwango hicho cha uzalishaji kimeiwezesha nchi
kujitosheleza kwa mahitaji yake ya chakula ya tani milioni 13.56 na hivyo kuwa
na ziada ya tani milioni 3.32 za chakula kwa kiwango cha utoshelevu cha asilimia
124.

“Niwahakikishie
watanzania kwamba, tunacho chakula cha kutosha nchini.  Hata hivyo,
tuendelee kuweka akiba katika kaya zetu hadi tutakapovuna tena kwani inaonekana
kwamba huenda tusiwe na mavuno mazuri sana msimu huu kutokana na uhaba wa mvua kwenye
maeneo ya Kanda ya Ziwa, Kati na Kaskazini mwa nchi yetu”. Amekaririwa Waziri
Hasunga.


Kuhusu kilimo cha umwagiliaji, Mhe. Hasunga alisema katika mwaka 2018/2019,
Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imekamilisha mapitio ya Mpango
Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2002 ili kubaini maeneo yanayofaa kwa
kilimo cha umwagiliaji kwa kuzingatia Mipango Shirikishi ya Maendeleo ya
Rasilimali za Maji.

Katika mpango
huo, hekta 560,880 zimepangwa kuendelezwa kwa lengo la kuongeza eneo la umwagiliaji
kutoka hekta 475,052 mwaka 2018/2019 hadi hekta 1,000,000 ifikapo mwaka 2035.


Waziri Hasunga ameuzungumzia Ushirika na kusema Wizara kupitia Tume ya
Maendeleo ya Ushirika imeendelea kuimarisha Sekta ya Ushirika kwa kusimamia na
kuhamasisha maendeleo yake. Vyama vya Ushirika vimeongezeka kutoka vyama 10,990
Desemba 2017 hadi vyama 11,331 kufikia Desemba 2018. Vilevile, idadi ya
wanachama wa vyama vya ushirika imeongezeka kutoka 2,619,311 mwaka 2017 hadi
3,998,193 Februari, 2019 sawa na ongezeko la asilimia 53.


Hadi Desemba 2018, mikopo yenye thamani ya Shilingi trilioni 1.3 imetolewa kwa
wanachama ikilinganishwa na Shilingi bilioni 902 iliyotolewa kufikia Desemba
2017.

Aidha, Akiba
na Amana za wanachama katika SACCOS zimefikia Shilingi bilioni 575 na hisa
Shilingi bilioni 79.