Pazzo, BMG
Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) tawi la Tanzania kwa kushirikiana na ile ya VIKES ya nchini Finland, imeandaa mafunzo ya kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kuwajengea uwezo wa kuripoti habari za kijinsia kwa weledi.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanafanyika jijini Mwanza kuanzia leo jumamosi Mei 18, 2019 yakiwashirikisha waandishi wa habari 25 kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Shinyanga pamoja na Simiyu.
Mkurugenzi wa MISA Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa amesema mafunzo hayo pia yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habati katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ili kuibua na kuripoti habari mbalimbali za kijinsia hususani zinazowagusa wanawake kwani wamekuwa hawapewi kipaumbele na vyombo vya habari.
“Tunahitaji kubadili fikra katika kuripoti habari za kijinsia, bado wanaume wanapewa kipaumbele huku wanawake wakisahaulika hivyo mafunzo haya yatusaidie kutoka tuliko na kuanza kuibua mambo mazuri yanayofanywa na wanawake na kuyaripoti kupitia vyombo vyetu vya habari”, amesisitiza Gasirigwa.
Akiwasilisha mada ya jinsia kwenye mafunzo hayo, Alex Mchomvu kutoka Chuo Kikuu cha SAUT Mwanza amesema baadhi ya mila na desturi zimekuwa zikiathiri masuala mbalimbali ya usawa wa kijinsia hivyo waandishi wa habari wanapaswa kutumia vyombo vya habari kubadili hali hiyo ili kuleta usawa kwenye masuala ya kijinsia.
Naye Kenneth Simbaya, Mwenyekiti Mtandao wa Waandishi wa Habari za Afya Tanzania (Africa Media Network on Health Accountability Tanzania Chapter), akiwasilisha mada kuhusu misingi ya uandishi wa habari amehimiza waandishi wa habari kuiishi misingi hiyo ikiwemo ukweli na usahihi bila kupendelea kwani wamepewa dhamana kubwa katika jamii.
“Kuna wasiwasi mkubwa kwa sasa juu ya utendaji wa wanahabari ambapo ukweli ni kwamba jamii haituamini tena. Lakini imani au kuaminika ni jambo la muhimu katika kazi yetu kama wanahabari” amesema Simbaya na kuongeza;
“Ili kurudisha imani hiyo ni lazima waandishi wa habari na vyombo vya habari kuiishi misingi au miiko ya wanahabari ambayo ni ukweli na usahihi, uhuru (kutokuwa tegemezi), kuzingatia usawa (fairness and impartiality), utu (humanity) na uwajibikaji (Accountability)” amesisitiza Simbaya.
Washiriki wameishukru taasisi ya MISA Tanzania kwa kuandaa mafunzo hayo wakisema yatawasaidia katika utendaji wao wa kazi ikiwemo kuandaa habari na makala mbalimbali kuhusu usawa wa kijinsia kwa kutoa nafasi sawa baina ya wanawake na wanaume tofauti na ilivyo sasa ambapo asilimia kubwa ya vyanzo vyao ni wanaume wakati kuna wanawake wengi wanafanya mambo makubwa lakini habari zao hazipati nafasi.