Na Judith Mhina -Maelezo
Adhima ya Tanzania kuwa kinara uuzaji wa dhahabu Afrika Mashariki na kuzuia utoroshaji ya madini yake imetimia.
Hii imetokana na kutekelezwa kwa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika kuratibu na kutambua madini yote, kuanzishwa kwa masoko ya ununuzi ya dhahabu ndani na uuzwaji wa madini nje ya nchi.
Kuzinduliwa kwa soko kuu la kimataifa la uuzaji wa madini ya dhahabu Mkoa wa Mwanza, lililopo katika jengo la Rock City Mall, kumedhihirisha nia ya Tanzania kuhakikisha inalinda rasilimali za madini ya Tanzania. Hii inawahakikishia wachimbaji wadogo kunufaika na kazi yao, pamoja kuchangia pato la Taifa.
Akiongoza utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli mapema mwezi Machi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa alizindua mnada wa dhahabu katika Mkoa wa Geita, yenye masoko mawili, ili kuondoa changamoto ya wachimbaji wadogo kuhangaika kutafuta mahali pa kuuzia madini yao.
Baadhi ya Mikoa iliyotekeleza agizo la ujenzi vituo vya kuuzia dhahabu ni pampja na Geita, Mwanza, Shinyanga, Chunya (Mbeya) Mpanda, (Katavi), Mara, Arusha, Singida, Iringa, Mkinga (Tanga) na Manyara ambao wanajenga vituo viwili vya kuuzia madini ya Tanzanite na vito vingine.
Aidha, ujenzi huo utajengwa katika miji midogo ya Mererani maalum kwa ajili ya uuzwaji wa madini ya Tanzanite na vito, wakati soko la pilli linajengwa mji mdogo wa Orkesumet kwa ajili ya uuzwaji wa ruby, green tourmaline na vito vingine.
Jitihada za Rais Magufuli za kulinda na kupigania rasilimali za Watanzania zimemfanya Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Museveni kutuma ujumbe ulioongozwa na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Peter Crolies, kukiri kuwa uwekezaji nchini Tanzania katika sekta ya madini ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine za Afrika.
Waziri Crories amesema hayo katika ziara ya siku nne mkoani Mwanza na Geita ambapo lengo ni kujifunza, jinsi Tanzania inavyoendesha sekta ya madini na kufanikiwa kuwa na uhusiano mzuri baina ya serikali, wachimbaji wadogo na wakubwa kwa kudumisha amani.
“Tanzania na Uganda zitaendelea kushirikiana katika Nyanja za kitekinolojia na taarifa za kiolojia Tumekuja hapa kujifunza jinsi ya usimamizi wa rasilimali ya madini ili nasi kupata ujuzi kutoka TZ ambao tutakwenda kufikisha jatika serikali yetu na kuwafundisha wananchi wetu wanaojihusisha na uchimbaji” Amesema Waziri Clories.
Amesema ziara hiyo imekuwa na mafanikio kwao kwa kuwa hajawahi kushuhudia na kujifunza rasilimali za madini zinavyotakiwa kuendeshwa na kutunzwa hadi kufikia hatua ya jamii na serikali wa kupata uchumi mzuri.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri wa Madini Stansilaus Nyongo amesema wachimbaji wadogo ndio watoroshaji wakubwa wa madini hususan dhahabu lakini Tanzania imejipanga kuthibiti na kupunguza namna ya utoroshwaji wa huo kwa kuanzisha masoko hayo ya kuuzia madini.
Watanzania wamekuwa na utamaduni au desturi ya kudharau na kubeza jambo lolote jema linaloanzishwa hapa nchini na kupenda kusifia na kuona mambo yanayofanyika nje ya Tanzania ndio mema tu. Waswahili husema “Mdharau kwao ni mtumwa”.
Lakini ubora wa Tanzania umethibitishwa na Waganda walioona ni vizuri kuja kujifunza kuhusu madini kutokana na nchi yetu kutunza vizuri rasilimali za madini hasa kwa wachimbaji wadogo. Ambapo imekuwa vigumu kwa nchi nyingine kufanya kazi kwa ushirikiano na kudumisha amani. Amesema Waziri Nyongo.
Ujumbe wa Uganda ulikuwa na maafisa waandamizi wa serikali pamoja na wachimbaji wadogo 35 ulitembelea maeneo yanayochibwa dhahabu katika migodi ya Geita Gold Mine– GGM Rwangwa Busonwa Mine, Msagano na maeneo ya kuchengulia dhahabu ya Rich Hill na Genge tatu.
Zoezi hili la uazishwaji wa vituo vya kuuzia madini ni utekelezaji wa maagizo kadhaa ya Rais Magufuli ambapo, itarahisisha serikali kuratibu wanunuzi wa madini na wanunuzi hao kujulikana wanapoyauza madini hayo, ndani na nje ya nchi, na kutambua kiasi cha fedha nchi ilizopata kutokana na mauzo hayo.
Aidha, kurejeshwa kwa utaratibu wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania-BOT, kuhusika na ununuaji na uuzaji wa dhahabu, iliyochenguliwa nje ya nchi na kuratibu mapato yatokanayo na uuzwaji wa dhahabu na madini mengine ambayo yanapatikana hapa nchini Tanzania. Itadhihirisha dhahiri kama nchi tunaongoza katika uuzaji wa dhahabu Afrika Mashariki.
Kulingana na taarifa ya mwezi April ya BOT kuna ongezeko la uuzwaji wa dhahabu nje ya nchi. Ongezeko hilo lililotokana na ulinzi na uangalizi sahihi wa uuzwaji wa madini ambapo watoroshaji walikuwa na mwanya wa kuiba katika migodi na kutorosha nje ya Tanzania.
Umakini wa serikali wa Awamu ya Tano umaezaa matunda katika migodi miwili mikubwa hapa Tanzannia ukiwemo Geita Gold Mining na North Mara Gold Mining baada ya kuzalisha kiasi kikubwa zaidi cha madini hayo na kuuzwa nje ya nchi .
Ongezeko hilo ni la Dolla za Marekani milioni 100 kuanzia Julai 2018, mpaka kuishia Machi 2019 ambapo ni sawa na fedha za Tanzania Bilioni 223. Ongezeko hilo ni la fedha za Marekeni ni sawa na bilioni 1.68 ikilinganishwa na mwaka 2018 mwezi Machi.
Pia, Mkoa wa Geita kilo 198 za dhahabu zimeuzwa kwa kipindi cha mwezi mmoja tangu soko hilo limeanzishwa tarehe 22 Machi mpaka April 2019. Vilevile Mkoa wa Mbeya Wilaya ya Chunya ndani ya siku nne tangu soko kuanzishwa, kilo 22 zimeuzwa wakati hapo nyuma zilirekosiwa kuuzwa kilo 12 tu kwa mwaka mzima.
Ongezeko hili la dhahabu kuuzwa nje ya nchi, imesababisha kukuza pato la bidhaa na huduma zitolewazo na nchi ya Tanzania zilizotolewa kuishia Machi 2019 kufikia Dola za marakani Milioni 8.5 kutoka milioni 8.4 dola za marekani kwa mwezi Machi 2018.
Soko la dhahabu la Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya lilofunguliwa tarehe 05 Mei 2019 na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila akifungua soko hilo amesema “ Serikali imejipanga kuhakikisha soko a madini linatatua changamoto kubwa zinazowakabili wadau wa sekta ya madini”
Ameongeza kwa kusema “Kwa kuanzia serikali imeanzisha soko la pamoja la madini ambalo litatoa fursa kuanzia mchimbaji mdogo mpaka mkubwa na kuuza dhahabu yake sambamba na kuwatafutia wanunuzi”
Aidha, wafanyabiashara wa Chunya waliomba serikali kuwahakikishia usalama wa mali zao –madini na fedha zao katika soko hilo lililofunguliwa mjini Chunya, lakini bado wana wasiwasi kuhusu usalama wao. Hivyo ni vema serikali kuimarisha ulinzi na usalama kwenye eneo la soko na kwenye migodi.
Pia wanaipongeza serikali kwa kuweka soko la pamoja la madini ambalo litatoa nafasi kila mfanyabiashara wa dhahabu kuwa kwenye ushindani wa bidhaa yake.
Akitoa kasoro kadhaa zilizokuwepo kwenye sheria ya madini ya mwaka 2007 na kanuni zake Rais Magufuli aliagiza kufanya marekebisho ya sheria ambayo yalifanyika mwaka 2018 na kuagiza kurekebisha kanuni zake wakati wa Mkutano Mkuu na Wadau wa Sekta ya Madini mapema Januari 2019.
Marekebisho hayo yalihusu utaratibu wa uchimbaji wa dhahabu ikiwemo kuweka kumbukumbu ya dhahabu inayopatikana na mauzo yake, na kusaidia kupata takwimiu sahihi. Vilevile kujua ukweli katika Afrika Mashariki nchi ipi inayoongoza kwa uuzwaji wa dhahabu na madini mengine.
Maagizo hayo ya Rais Magufuli yalitolewa wakati wa mkutano wa wadau wa madini uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere-JNCC uliofanyika kuanzia tarehe 22 Januari mpaka 24, Januari 2019 Jijini Dar-es-salaam.
Hata hivyo, zipo changamoto mbalimbali za madini ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi kwa kutoa elimu ya kutosha kwa wadau ili serikali iweze kufanya kazi kwa pamoja na wananchi – wachimbaji wadogo wadogo na migodi mikubwa ya wawekezaji.
Mfano hivi karibuni Wilaya ya Gairo Mkoa wa Morogoro wachimbaji wa madini kadhaa na mmliiliki wa madini wamewakimbia viongozi ambao ni Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula ambaye alifatana na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Seriel Mchembe na Kamishina wa Tume ya Madini Dkt. Athanas Machiyeke.
Wadau hao waliacha madini aina ya Ruby, Nut, pikipiki na vitendea kazi baada ya kuona wanamiliki madini hayo kinyume cha sheria bila kuwa na kubali cha kumiliki. Hii ni uthibitisho kuwa sekta ya madini bado inahitaji ushirikishaji wa karibu wa wadau ili wajue wajibu wao wa kufata sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya sekta husika.