Na Mwandishi wetu, Mihambwe
Wakandarasi wanaoshinda kandarasi za ujenzi wametakiwa kuacha urasimu na ubabaishaji kwenye utekekezaji wa kazi wanazolipwa na Serikali na miradi yote itakayokosa ubora wa viwango isipokelewe.
Ameeleza si busara kwa kampuni za ujenzi zilizopitishwa chini ya taratibu za kisheria, kushinda zabuni na kulipwa fedha za umma zishindwe kujenga kwa viwango na kumaliza kwa wakati.
Msimamo huo umetolewa na Gavana Emmanuel Shilatu alipokagua ujenzi miradi ya ofisi, soko na choo katika kiijiji cha Ngongolo kata ya Miuta.
Shilatu alisema Wakandarasi wana wajibu wa kutimiza ahadi kama mikataba yao ilivyoeleza, kujenga majengo kumaliza kwa wakati husika kazi zao bila visingizio vyovyote.
“Tabia za uzembe na ubabaishaji mkubwa wa ujenzi chini ya kiwango na miradi mingine kutokuanza kabisa licha ya Mkandarasi kupewa pesa tangu Septemba 2018 inatakiwa ife.
“Ifike mahali uzalendo utusute na kuona aibu. Tuheshimu fedha za umma na kusimamia matumizi bora. Hatuwezi kupata maendeleo ikiwa tutaongozwa na uzembe au ubadhirifu. Miradi ambayo itakosa kujengwa kwa viwango isipokelewe.” Alisema Gavana Shilatu
Aidha Gavana huyo alitoa agizo kwa Mkandarasi wa ujenzi huo akimtaka kufika kazini mapema na kuiasa Serikali ya Kijiji pamoja na kamati ya ujenzi kuwa makini katika usimamizi miradi ya maendeleo.
Katika ziara hiyo Gavana Shilatu aliambatana na Mtendaji Kata Miuta, Serikali Kijiji cha Ngongolo pamoja na kamati ya ujenzi Kijiji cha Ngongolo.