Home Mchanganyiko JESHI LA POLISI LAWAKAMATA WATU NANE WANAODAIWA KUIBA MALI YENYE THAMANI YA...

JESHI LA POLISI LAWAKAMATA WATU NANE WANAODAIWA KUIBA MALI YENYE THAMANI YA MIL. 300 YA KAMPUNI YA ORGANIA PRODUCTION KIBAHA, PWANI-WANKYO

0
NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA
JESHI la polisi mkoani Pwani, linawashikilia watu nane wanaodaiwa kuhusika na wizi wa mashine za kutotoloshea vifaranga vya kuku,mashine ya maji, mfumo wa umeme na vyuma mbalimbali vya uzalishaji zenye thamani ya milioni 300, mali ya kampuni ya organia production ltd,iliyoko huko Boko Mnemela Kibaha Pwani.
Kamanda wa polisi mkoani hapo, Wankyo Nyigesa amewaambia waandishi wa habari kuwa, mara baada ya kupata taarifa kutoka kwa meneja wa ulinzi wa kampuni hiyo Ismail Yahaya, walifuatilia kwa kutumia kikosi maalum cha askari wa jeshi la polisi.
Alieleza, mei 13 mwaka huu walimkamata Musa Omary (17),Abdallah Salehe  (14) na William Pius (15) wakazi wa Pichandege wakiwa na pikipiki yenye namba za usajili MC. 640  CBF aina ya Haojue iliyobeba vyuma ambavyo ni mali iliyoibiwa mei 12 katika kampuni hiyo.
Baada ya kuendelea na upelelezi mei 14 jeshi hilo lilimkamata Dotto Said (28) ,Martin Michael (35),Mshamu Nassoro (25) na Ramadhani Dossa (25),wakazi wa Pichandege ambao nao wameshiriki kwenye wizi huo.
“Tumemkamata mtuhumiwa Joseph Mwakasuka mkazi wa Mailmoja, Kibaha ambae ni mnunuzi wa vyuma chakavu ambapo amekamatwa na vyuma mbalimbali vinavyohusiana na mashine ya kutotolea vifaranga vya kuku, cooper wire zilizokuwa ndani ya mfuko, box za control panel nne na mifuniko ya sinki za maji “aliweka bayana.
WAKATI HUO HUO -Emmanuel Yusuph (36) mkazi wa Chanika Dar es salaam ameuawa na watu wanaodhaniwa ni watumishi wa idara ya misitu Kisarawe.
Alisema kuwa, kabla ya tukio hilo marehemu na mwenzake John Mwaluko mkazi wa Pugu Kajiungeni alijeruhiwa na watumishi hao kwa kukatwa miguu yote na kitu chenye ncha kali baada ya kukutwa wakichoma mkaa katika msitu huo.
Wankyo alifafanua, mara baada ya jeshi hilo kupokea taarifa hiyo askari walifika eneo la tukio kwa ajili ya uchunguzi ambapo walifanikiwa kuwakamata Lameck Samamba (28) askari ulinzi wa misitu mkazi wa Kisarawe na Regina Mwakifuna (29)ambae ni ofisa misitu msaidizi.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospital ya wilaya ya Kisarawe na majeruhi anapatiwa matibabu hospitalini hapo.