Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome (katikati) akizungumza kufungua kikao cha kuandaa Mpango kazi wa pili wa kitaifa wa haki za binadamu kinachofanyika mjini Singida.
Wajumbe wa kikao cha kuandaa Mpango kazi wa pili wa kitaifa wa haki za binadamu wakimsikiliza Katibu Mkuu Prof.Mchome wakati akifungua kikao hicho
…………………
Wadau wa kuandaa Mpango Kazi wa Pili wa Kitaifa wa Haki za Binadamu 2019-2023 wanakutana kama kamati kupitia maoni ya mtaalamu mshauri kwa ajili ya kuandaa mpango huo.
Kikao hicho kinafanyika mjini Singida kimefunguliwa na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome ambaye amewatakawadau hao wahakikishe wanatoka na vitu vichache vinavyotekelezeka na ambavyo vitatoa picha nzuri ya utekelezaji kwa nchi.
“Tusiwe na mambo mengi ambayo yatakuja kuleta shida katika utekelezaji,mkumbuke kuwa suala la haki za binadamu lina vitu vingi sana, tujipange kwa yale ambayo yatatuwezesha kutoka na taarifa bora ya utekelezaji wetumbele ya dunia,” alisema Prof. Mchome
Amesema suala la kukuza na kulinda haki za binadamu ni suala la msingi ambalo Serikali inatekeleza ikizingatiwa makubaliano ya kimataifa ambayo kama nchi iliyaridhia.
Mpango Kazi wa Haki za Binadamu utawezesha vipaumbele vya nchi kuhusu masuala ya haki za binadamu kujulikana, pamoja na kubainisha namna ya kutekeleza katika kukuza, kulinda na kuendeleza haki za binadamu nchini.
Zoezi la uandaaaji wa Mpango Kazi wa Pili wa Kitaifa wa Haki za
Binadamu lilianza Oktoba 2018 ambapo Wizara ya Katiba na Sheria, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa Kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Kimataifa kupitia Wataalamu Waelekezi walikusanya maoni kutoka kwa makundi mbalimbali wakiwemo Wadau kutoka Serikali za Mitaa; Wadau Kutoka Taasisi za Kidini; Asasi za Kiraia, Vyombo vya Habari; na Wananchi ili kupata vipaumbele vya kuingiza katika Mpango
Kazi huu.
Mpango Kazi wa Kwanza wa Kitaifa wa Haki za Binadamu wa 2013-2017 ulimalizika 2018.