Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Bi. Consolata Mushi (kulia) akifafanua jambo kwa Mgeni Rasmi Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni toka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu wakati wa hafla fupi ya kumtunuku cheti cha ujuzi wa lugha ya Kiswahili Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni (katikati) mapema hii leo katika Ofisi za BAKITA jijini Dar es Salaam.
Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni toka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu (kushoto) akizungumza na watumishi wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) hawapo pichani wakati wa hafla fupi ya kumtunuku cheti cha ujuzi wa lugha ya Kiswahili Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni (kulia) mapema hii leo katika Ofisi za BAKITA jijini Dar es Salaam.
Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni toka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu (kushoto) akimkabidhi cheti cha ujuzi wa lugha ya Kiswahili Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni (kulia) Wakati wa hafla fupiiliyofanyika mapema hii leo katika Ofisi za BAKITA jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni (kulia) akitoa neno la shukrani kwa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kwa kumtunuku cheti cha ujuzi wa lugha ya Kiswahili mara baada ya kumaliza mafunzo.
Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni toka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emmanuel Temu (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni (wapili kulia) na watumishi wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) mara baada ya kumtunuku balozi huyo cheti cha ujuzi wa lugha ya Kiswahili mapema hii leo katika Ofisi za BAKITA jijini Dar es Salaam.
Picha na WHUSM – Dar es Salaam
****************************************
Na. WHUSM – Dar es Salaam
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limemtunuku cheti cha ujuzi wa lugha ya Kiswahili Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni mara baada ya kumaliza mafunzo na kufaulu katika ngazi ya kati.
Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi za BAKITA jijini Dar es Salaa, Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni toka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Emanuel Temu amempongeza Balozi huyo na kuwaomba wanadiplomasia wengine kujifunza lugha ya Kiswahili kwani itawasaidia katika shughuli mbalimbali wakiwa hapa nchini.
“Nikupongeze Mheshimiwa Balozi kwa jitihada ulizozionesha na kuweza kumaliza mafunzo ya lugha ya Kiswahili na leo hii tunakutunuku cheti rasmi cha ujuzi wa lugha ya Kiswahili naamini hata ukirudi nchini Italia utaendelea kuwa balozi wa kueneza lugha ya Kiswahili nchini Italia na nitoe wito kwa wanadiplomasia wengine waje BAKITA kujifunza lugha ya Kiswahili,” alisema Dkt. Emanuel Temu
Nae Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Bi. Consolata Mushi amempongeza Balozi Mengoni kwa kuweza kumaliza mafunzo yake pamoja na kuwa na majukumu mengine mengi.
“Ndugu Mgeni Rasmi kwa sasa wanadiplomasia wameonesha muamko wa kujifunza lugha ya Kiswahili kwani mpaka sasa Balozi wa Italia ni wa pili kutunukiwa cheti cha ujuzi wa kugha ya Kiswahili akitanguliwa na Balozi wa Polandi nchini Tanzania Mheshimiwa Krzysztof Buzalski,” alisema Bi. Consolata.
Kwa upande wake Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni ametoa shukrani kwa BAKITA kumuwezesha kujifunza na kuelewa lugha ya Kiswahili kwani Mabalozi wengi hutumia lugha ya Kiingereza na kuwa ngumu kwao kufanya mawasiliano kwani asilimia kubwa ya Watanzania wanazungumza Kiswahili kuliko kiingereza.