Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge akizungumza na wajumbe wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) kikao cha kupitia tathmini na kuweka mipango mipya ya utekelezaji katika Mkoa wa Dodoma.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bwana Joseph Mafuru akifafanua jambo kwa wajumbe wa kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) kikao cha kupitia tathmini na kuweka mipango mipya ya utekelezaji katika Mkoa wa Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma Dkt Suleiman Serera akichangia hoja katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) kikao cha kupitia tathmini na kuweka mipango mipya ya utekelezaji katika Mkoa wa Dodoma.
Mbunge wa Jimbo la Mvumi Mheshimiwa Livingston Lusinde akichangia hoja katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) kikao cha kupitia tathmini na kuweka mipango mipya ya utekelezaji katika Mkoa wa Dodoma.
***********************************
Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amewataka Wakuu wa Wilaya na Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma kutengeneza mikakati ya kuhakikisha wanajenga vyumba vya madarasa ili kukabiliana na upungufu wa madarasa uliopo unaosababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kuripoti masomoni.
Dkt Mahenge ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa(RCC), baada ya kubaini kuwa kuna upungufu wa vyumba 148 vya madarasa kwa Mkoa mzima wa Dodoma huku Halmashauri pekee ya Kondoa mji ikiwa haina upungufu wa madarasa.
“Upungufu huu ni mkubwa sana nizitake Halmashauri zote zipange mikakati ya ndani mkisimamiwa na Wakuu wa Wilaya hakikisheni madarasa yanajengwa watoto walipoti shuleni” amesema Dkt Mahenge.
Aidha ameagiza Halmashauri kusimamia na kuweka misingi bora ya kuhakikisha wanaboresha elimu inayotolewa katika maeneo yao ametaka wanafunzi wanapomaliza masomo yao wawewamejengwa kimisingi ambapo wataweza kushindana katika soko la ajira.
“Elimu inayotolewa iwe na misingi iliyojengwa imara sio iliyojengwa kwa kutegemea mtu ambapo mtu huyo akihama na ufaulu unashuka hapana tunapotaka kupandisha ufaulu tuweke misingi iliyo bora” amesema.
Amewataka watumishi Halmashauri zote kwenda kufanyia kazi yale yote waliyokubaliana kwa sababu kila mtumishi ameelewa mipango waliyoipanga kama Mkoa, na amewataka kwenda kushirikiana na kushirikishana kwa ngazi zote ili kufikia malengo.
Ameitaka Wakala wa huduma ya misitu TFS Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanasimamia ajanda ya upandaji miti kwa Halmashauri zote na kujenga utaratibu wa kutembelea na kukagua zoezi hilo mara kwa mara na Wakuu wa Wilaya kusimamia zoezi hilo.
Ametoa onyo kwa Halmashauri zote zenye watumishi wenye tabia ya kuharibu mashine ya kukusanya mapato(Posi Mashine) amesema ataunda kamati maalumu ya kwenda kuchunguza mashine zote ambazo hazifanyi kazi na kusababisha upotevu wa mapato.
“Hizi Posi zisimamiwe kikamilifu katika maeneo yote na wale ambao waliagiza mashine ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI wafuatilie mapema zoezi limeishia wapi, isije kuwa kisingizio cha kuendelea kufuja mapato” amesema.
Amezitaka Halmashauri kwenda kusimamia ajenda ya kilimo na hasa wajikite katika mazao ya mda mrefu kama Zabibu, Korosho, Parachichi na Maembe sambamba na mazao ya chakula kuhakikisha kila Wilaya inajitosheleza kwa chakula.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Dodoma Bwana Godwin Mkanwa amewataka watendaji katika Halmashauri zote kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ilani ya Chama hicho kwani ndio mkataba baina ya Serikali na wananchi.
Amesema kamati ya siasa ya Mkoa ndio yenye dhamana ya kukagua miradi inayotekelezwa katika Mkoa husika hivyo wao watahakikisha wanapita kila mradi unaotekelezwa kuona kama yaliyoahidiwa yanatekelezeka na hawata sita kuwatolea taarifa wale wate ambao hawatasimamia ipasavyo miradi hiyo.