**************
TANGANYIKA
Afisa ushirika wa wilaya ya Tanganyika Luxford Mbunda na wajumbe wawili wa bodi ya chama cha msingi cha Ushirika Mpandakati Amcos wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Katavi kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za kununua na kuuza tumbaku nje ya mfumo wa vyama vya ushirika.
Wajumbe wa bodi wanaoshikiliwa na jeshi la polisi kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Zuberi Homera ni Makamu mwenyekiti wa chama Mashaka Shabani na mjumbe Leonard Joseph ambapo wamekamatwa wakati wa mkutano maalumu wa chama hicho ambao umefanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Ifukutwa .
Aidha,Bw.Homera amewataka viongozi wote wa bodi ya chama kuripoti jeshi la polisi na kupelekwa TAKUKURU kwa ajili ya tuhuma zinazowakabili.
Hata hivyo wanachama 6 Bw.Ramadhani Nassoro,Daniel Mnyema, Bakari Kaliso,Omari Kassimu,Kampojojo Kambobe na Laurent Kanikile waliokuwa wamefukuzwa uanachama mwaka 2018 wametakiwa kuandika barua ya kuomba kurejea katika chama na kutakiwa kutodai pesa waliyokuwa wakidai msimu wa kilimo mwaka 2016/2017.
Kikao hicho kilikuwa na lengo la kurejesha ripoti ya timu ya uchunguzi kuhusu malalamiko ya wanachama kukidai chama shilingi milioni 315 za mauzo ya tumbaku na shilingi milioni 170 zinazodaiwa kupotea katika mikono ya meneja wa Saccos ya chama aliyetoroka mwaka mmoj ana nusu uliopita.