*************************************
Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Jumuiya ya wahitimu wa chuo kikuu cha Dodoma UDOM imezunduliwa rasmi katika chuo hicho huku makamu Mkuu wa Chuo Profesa Faustine Bee akihimiza wahitimu kujiunga na umoja huo ili kupata fulsa mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uzinduzi huo Prof. Bee amesema ni vema kwa wahitimu wa Chuo hicho kujiunga na jumuiya hiyo kwa lengo la kubadilishana mawazo na kushirikishana katika fulsa mbalimbali.
” Ni muhimu kwa wahitimu kujiunga na jumuiya hii humu kuna wafanyabiashara, wafugaji wa kuku, mbuzi na wengine wanafanyakazi katika maeneo mbalimbali” amesema Prof. Bee.
Aidha amesema kuwa wahitimu hao ni watu muhimu kwa maendeleo ya Chuo hasa katika ujenzi wa majengo ya shule ununuzi wa computer ununuzi wa vitabu na vitu vingine vingi vinavyowahusu wanafunzi ambavyo vimekuwa ni changamoto Chuoni hapo.
“Ili ni jambo la kawaida na ni jambo jema katika vyuo vyote kuwakusanya wahitimu wote na watumishi katika kujadili changamoto na kuona ni namna gani wanazitatua “amesema Profesa Bee.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa umoja huo Dkt Paul Loisulie amesema lengo la jumuiya hiyo ni kuwaweka wahitimu pamoja kusaidia na kutengeneza Maendeleo mazima ya Chuo ambacho wamesoma.
Amesema tayari wameshaandaa katibu ya jumuiya hiyo na wapo katika mchakato wa kutafuta wahitimu ambao wanakadiliwa kufikia elfu hamsini na sita(56) ambapo kwa sasa inawanajumuiya 1000, malengo yao ni kuwa umoja huo uwe wa mfano katika Jumuiya nyingine.
Amesema moja ya malengo ya umoja huo ni kupata mrejesho wa wahitimu hao ambao wapo maeneo mbalimbali kama elimu wanayoipata chuo kama inaendana na uhalisia wa maisha na kazi wanazozifanya.
“Chuo hiki wamemaliza wanafunzi wa kada mbalimbali wapo wanasheria, walimu na kozi mbalimbali tunatamani kupata mrejesho elimu hii inawasaidia au marekebisho gani yafanyike katika mfumo wetu wa elimu” amesema.