Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji limefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 57 wote raia wa Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Ni kwamba mnamo tarehe 15.12.2020 majira ya saa 18:00 jioni, Jeshi la Polisi lilipata taarifa toka kwa raia wema kuwepo kwa watu wanaowatilia mashaka huko Kijiji cha Bulongwe kilichopo Kata ya Masoko, Tarafa ya Pakati, Wilaya ya Rungwe na kisha kufanya ufuatiliaji na ndipo tulifanikiwa kuwakamata raia 57 wa Ethiopia pamoja na wenyeji Watanzania wawili ambao ni EDOM MWANDUSU [37] na DAUDI MAGEHEMA [34] wote wakazi wa Bulongwe.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako mkali dhidi ya mawakala wa usafirishaji wahamiaji haramu ambao wamekuwa wakifanya biashara hiyo haramu. Ninatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu au wahalifu ili tuweze kuchukua hatua haraka zaidi.
Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawatafuta watu wawili ambao ni mawakala wa usafirishaji wahamiaji haramu ambao ni:-
- OBEDI MPIKI MWAKAPUSYA, Mkazi wa Rungwe na Kyela na
- MANENO ambaye ni mkazi wa Uyole Jijini Mbeya.
Oktoba 30, 2020 huko Lunwa Wilaya ya Mbarali, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilikamatwa raia 22 wa Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila kibali. Huu ni muendeleza wa operesheni na misako inayofanywa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya.
KUPATIKANA NA DAWA ZA KULEVYA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya mnamo tarehe 15.12.2020 limeendelea na misako dhidi ya wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya aina ya Bhangi katika maeneo ya Itumbi Wilaya ya Chunya, Ubaruku Wilaya ya Mbarali na Chapakazi Mji Mdogo wa Mbalizi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na dawa za kulevya aina ya Bhangi gramu 560.
Watuhumiwa waliokamatwa katika misako hiyo ni:-
- KAPTA JOHN @ MWAKALANJE [40] Mkazi wa Itumbi.
- SAID ISMAIL @ CHOVYA [37] Mkazi wa Igawa – Lugelele.
- PASCHAL PAULO MAPUNGILO [34] Mkazi wa Chapakazi.
Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
KUPATIKANA NA POMBE HARAMU YA MOSHI [GONGO].
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu 1. ABDALAH MWAKALISYA [33] 2. LUSAJO PAUL [35] na 3. MANENO MALAKI [24] wote wakazi wa Kijiji cha Ibililo Wilaya ya Rungwe wakiwa na Pombe Haramu ya Moshi lita 34.
Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 15.12.2020 majira ya saa 13:30 mchana huko Kijiji cha Ibililo kilichopo Kata ya Nkunga, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya katika misako inayoendeshwa na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya.
Imetolewa na:
[ULRICH O. MATEI -SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.