Na John Walter-Manyara
Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kushirikiana na ofisi ya Mtakwimu mkuu wa serikali Zanzibar na shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN women) pamoja na shirika la maendeleo la kiuchumi wanatarajia kufanya utafiti wa masuala ya kijinsia mila,desturi,sheria na Tamaduni za Tanzania kwa mwaka 2020.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo yanayoendelea katika mji wa Babati Mkoani Manyara kwa Wadadisi na Wasimamizi wa utafiti wa masuala ya jinsia ,mila,desturi sheria na utamaduni mwakilishi kutoka ofisi ya takwimu na sensa Rose Minja kwa niaba ya mtakwimu mkuu wa serikali Dkt Albina Chuwa alisema Lengo kuu la utafiti huo ni kukusanya takwimu ambazo zitasaidia kupima uelewa wa watu kuhusiana na mila ,desturi sheria na utamaduni zinazoweza kuleta ukosefu wa usawa wa kijinsia na uwepo wa ubaguzi katika sekta mbalimbali za jamii kama vile ajira ,afya na elimu umiliki wa rasilimali na biashara.
Alisema Malengo mengine ni pamoja na kupata takwimu zinazobainisha ubora wa mifumo ya kisheria na mipango ya kulinda haki za wanawake na kukuza usawa wa kijinsia na kuwezesha utengenezaji wa kanzi data inayojumuisha viashiria vya msingi vya kiwango cha ubaguzi katika sheria mila na desturi.
Alieleza kuwa Matokeo ya utafiti huo yanatarajiwa kuchochea kasi ya maendeleo endelevu nchini,kasi ambayo itajidhihirisha katika tathimini ya utekelezaji ya mipango mbalimbali ya maendeleo serikali iliyojiwekea katika ngazi za kimataifa ,kikanda na kitaifa .
Alisema jumla ya wataalam 74 kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wamekutana Mkoani Manyara ambapo wanatarajia kufanya utafiti huo katika maeneo 217 ya Tanzania ambapo maeneo 182 na 35 yatakuwa Zanzibar.
Pamoja na hayo alisema utafiti huo unatarajia kufanyika katika kaya 4,340 nchi nzima ambazo zitachaguliwa kisayansi ili kupata sampuli wakilishi huku utafiti huo ukifanyika pia kwa watu binafsi wapatao 8,680 wakiwemo wanawake 4,340 na wanaume 4,340 ambapo muundo huo unaelezwa kusaidia kutoa matokeo katika ngazi ya muungano kitaifa na kimkoa .
“Matokeo ya utafiti huu yatakusaidia kuendelea kupanga mipango sahihi itakayojumuisha jumla ya wanawake 931,976 na wanaume 941,129 walioko mkoani kwako kwa mjibu wa makadirio ya idadi ya watu ya mwaka 2020 kwa kuwa 83% ya wakazi wa Mkoa wako wanajihusisha na kilimo na ufugaji na matokeo haya yataweza kubaini hali halisi ya umiliki wa ardhi ikiwa ni pamoja na ni nani mwenye haki ya kutumia ardhi yenye dhamana na uwepo wa nyaraka za umiliki”alisema Bi. Rose
Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Misaile Mussa alisema utafiti huo utasaidia kujua mbinu mpya zinazotumika katika masuala ya ukatili wa kijinsia na wanawake hususani mkoani hupo.
“Taarifa bora na makini itatusaidia wengine kuleta matokeo bora kwani lengo ni kutathimini na kufatilia malengo endelevu kuhusu usawa wa kijinsia na uwezeshwaji kwa wanawake kiuchumi”alisema Mussa.
Naye mtaalam wa programu ya wanawake kutoka umoja wa mataifa Dr. Sadananda Mitra alisema umoja wa mataifa umeamua kusaidia utafiti huo ili kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za ukatili wa kijinsia na serikali kuweza kupanga mipango endelevu ikiwa ni pamoja na kuthibiti vitendo hivyo.