………………………………………………………………….
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dk.Jim Yonazi amepongeza juhudi za Huawei za kuboresha ubora wa elimu ya ICT ili kuongeza ujuzi wa kuajiriwa kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Tanzania.
Dk Yonazi alitoa pongezi hizo wakati wa Sherehe za Ufunguzi wa msimu wa tano wa programu ya “Seeds for the Future” ambao ulifanyika mtandaoni mapema wiki hii.
Kwa mara ya kwanza hapa nchini, programu ya “Seeds for the Future” ilizinduliwa mnamo 2016 kwa msaada wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Programu hiyo ilihusisha Vyuo Vikuu 4 wakati ikizinduliwa na sasa inajumuisha Vyuo Vikuu 7 ambavyo ni Chuo Kikuu ya Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT ) na Chuo Kikuu cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE)
“Nimearifiwa kuwa katika kuchangia ukuzaji wa vipaji vya TEHAMA nchini Tanzania na kuendana na mipango ya kimkakati ya nchi, Huawei imeongeza kwa kiasi kikubwa shughuli na ushirikiano na Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu hapa nchini. Hizi ni juhudi za kupongezwa kwa kwa kuwawezesha vijana wa kitanzania. ” Dkt. Yonazi wakati akitoa hotuba yake kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Zainab Chaula.
Pia, Dk Yonazi amewataka wanafunzi kutumia maarifa wanayopata kwenye programu hiyo kufundisha wengine ili kufaidisha idadi kubwa ya watu haswa wale ambao hawakuwa na bahati kama wao.
“Nawapongeza wanafunzi wote ambao wameshiriki katika program ya Seeds for the Future mwaka huu. Nawashauri watumie fursa hii ipasavyo kukuza maarifa yao na kupata uzoefu wa vitendo katika TEHAMA. Ninawahimiza pia kushiriki uzoefu waliopata na wenzao ili kuendeleza na kunoa maarifa waliyoyapata.” Aliongeza
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei Tanzania, Frank Zhou aliangazia mipango ya Huawei ya kuiwezesha Tanzania kukabiliana na mahitaji ya teknolojia kidijiti ambayo yanabadilika mara kwa mara.
“Tunafahamu kuwa maendeleo ya dijiti yanahitaji mipango madhubuti ili kuiwezesha Tanzania kiuchumi kwa siku zijazo. Katika zama hii mpya, ujuzi wa TEHAMA utakuwa muhimu kwa jamii, kwa mashirika, na muhimu zaidi kwa vijana. Ndio maana tumewekeza kwa kina katika mipango kadhaa haswa ukuzaji wa vipaji zna ujuzi.” Alisema.
Mwaka huu, ili kufikia vijana wengi zaidi nchini Tanzania, Programu ya “Seeds for the Futrure” itafanyika mtandaoni ili iweze kuchukua idadi kubwa ya wanafunzi kutoka mikoa tofauti na ili wanafunzi wenye mahitaji maalum pia washiriki. Ikilinganishwa na miaka ya nyuma, Huawei imeweza kuongeza idadi ya nafasi za mafunzo kutoka wanafunzi 10 hadi 47.
“Ninajivunia kuwatangazia kwamba baadhi ya washiriki hao ni wanawake, ambao wana nafasi muhimu sana katika tasnia ya TEHAMA. Ninapenda kuhamasisha wanafunzi wengi wachanga wanaohudhuria kozi hiyo kuangalia na kuijikita zaidi katika tasnia ya Mawasiliano.” Aliongezea
Kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Habari, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk. Leonard aliisifia program ya “Seeds for the Future” na nafasi yake katika kuwawezesha vijana na kukuza uwezo wa kuajiriwa.
“Programu hii ni mfano madhubuti wa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Huawei Tanzania katika kujenga mazingira yenye afya na endelevu ya rasilimali watu katika TEHAMA. Programu ya “Seeds for the Future” inafanya kazi kama daraja ambalo linaunganisha pengo lililopo kati ya mafunzo ya kinadharia na mahitaji ya vitendo katika soko la ajira. ”Alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha teknolojia wa Airtel, Bwana Prosper Mafole aliwahimiza wanafunzi kutumia fursa za kujifunza zinazotolewa na Huawei na akawakaribisha kwa msaada wowote endapo watahitaji.
Bwana Yuan Lin, Mshauri wa Uchumi na Biashara wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, ameipongeza kampuni ya Huawei kwa kuonesha mfano mzuri katika kukuza vipaji vya TEHAMA nchini Tanzania kwa kuwajengea uwezo vijana wa shahada ya kwanza ambao watakuwa msukumo wa mabadiliko ya TEHAMA nchini Tanzania katika siku za usoni.
“Ubalozi wa China nchini Tanzania unahimiza makampuni mengine ya China kuwa na mipango kama hii ili kusaidia katika kuandaa wataalamu ambao wanasimama imara katika kutimiza malengo ya Tanzania ya uchumi wa viwanda na kuwa nchi ya kipato cha kati.” Alisema.
Sherehe ya ufunguzi wa “Seeds for the Future” ilihudhuriwa na maafisa wa Serikali mashuhuri wakiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, na Mshauri wa Uchumi na Biashara wa Ubalozi wa China nchini Tanzania Bwana Yuan Lin.