Muonekano wa ujenzi wa jengo la maabara ya uvuvi litakalotumika na Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) linalojengwa kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH), jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah (katika) akiongozwa na Mratibu wa Mradi wa SWIOFISH Bw. Nichrous Mlalila (Kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la maabara linalotakiwa kukabidhiwa kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi tarehe nane mwezi Desemba 2020.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah akikagua moja ya maeneo ya jengo la maabara ya uvuvi linalojengwa kupitia mradi wa SWIOFISH katika ofisi za Taasisi ya Utafiti Tanzania (TAFIRI) jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa ndani wa moja ya maeneo ya jengo la maabara ya uvuvi litakalotumika na Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) linalojengwa kupitia mradi wa SWIOFISH.
………………………………………………………………………………….
Na. Edward Kondela
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema serikali imetilia mkazo suala la utafiti katika sekta ya uvuvi nchini ili kuhakikisha inapata taarifa sahihi ya maeneo ya mavuvi, kuzalisha vifaranga bora vya samaki pamoja na chakula bora cha samaki.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa maabara ya kisasa ya utafiti wa uvuvi itakayotumika na Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) inayojengwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH), Dkt. Tamatamah amesema mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa mkopo wa masharti nafuu wa Shilingi Bilioni 2.6 unalenga kukuza sekta ya uvuvi nchini.
“Kwenye uchumi wa bluu katika awamu hii tunategemea meli nane kwenye uvuvi wa bahari kuu hivyo unapofanya uvuvi wa bahari kuu haujiendei tu lazima watafiti kama TAFIRI waende baharini wajue chambo wanapata wapi kwa ajili ya kuvua samaki, pia tuna mpango wa kuongeza uzalishaji wa samaki kupitia ufugaji kwenye maeneo mawili ya chakula bora pamoja na vifaranga bora hivyo tafiti ni muhimu kupitia maabara hii.” Amesema Dkt. Tamatamah
Ameongeza kuwa katika miaka mitano ijayo serikali itapunguza au kuondoa kabisa changamoto ya upatikanaji wa vifaranga bora vya samaki na chakula bora cha samaki kutokana na watu wengi kujitokeza katika ufugaji wa samaki ambapo mahitaji ni vifaranga milioni 50 kwa mwaka lakini kwa sasa vifaranga vinavyozalishwa hapa nchini ni milioni 30 pekee.
Kwa upande wake mratibu wa mradi wa SWIOFISH Tanzania Bara Bw. Nichrous Mlalila amesema baada ya kukamilika kwa jengo hilo wataalamu watajikita katika kufanya utafiti ambapo kwa sasa sampuli za mazao ya samaki zimekuwa zikisafirishwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya tafiti hali ambayo inahatarisha usalama wa nchi na rasilimali zake.
Aidha, amesema serikali inatarajia kujenga maabara nyingine kupitia mradi huo kwa ajili ya kuzalisha vifaranga bora vya samaki wa baharini pamoja na mbegu za zao la mwani katika kukuza sekta ya uvuvi hapa nchini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (TAFIRI) Dkt. Ismael Kimirei amesema taasisi hiyo ina mikakati mingi katika kukuza tafiti za uvuvi hapa nchini kwa kutumia teknolojia ya kisasa pamoja na kupunguza gharama za kutuma sampuli za uvuvi kwenda nchi za nje na hivyo sampuli zote kufanyiwa kazi katika maabara hiyo.
Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia umeanza kazi hapa nchini mwezi Juni mwaka 2015 na unatarajia kukamilika mwezi Mei mwaka 2021, huku serikali ikiwa na matumaini makubwa ya mradi huo kuendelea kuwepo hapa nchini kutokana na matokeo chanya katika kukuza sekta ya uvuvi kupitia mradi huo, ambapo ujenzi wa maabara hiyo unatarajia kuwa umekamilika na kukabidhiwa kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi tarehe 8 mwezi Desemba mwaka 2020.