************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Mahakama Kuu kwa kushirikiana na mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya nchini na ofisi ya mwendesha mashtakaa-DPP wameteketeza zaidi ya kilo 100 za dawa za kulevya ikiwemo heroini, cocaine na bangi ambazo kesi zake zimemalizika kwa kipindi cha miaka miwili na watuhumiwa kuhukumiwa.
Tukio la uteketezaji limefanyika Leo jijini Dar es Salaam katika kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill-TWIGA CEMENT ambapo zoezi zima lilifanyika kwa ulinzi wa jeshi la Polisi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika tukio hilo, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Jaji Edwin Kakolaki amesema baada ya kesi kumalizika mahakama hutoa kibali cha kuteketeza Vielelezo na zoezi hilo linaendeshwa kwa uwazi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali.
“Uendeshaji wa tukio hili kwa uwazi husaidia kuandoa dhana inayoenezwa mtaani kuwa dawa za kulevya hurudishwa tena mtaani baada ya kukamatwa”. Amesema Jaji Kakolaki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka nchini-DPP, Biswalo Mganga ameeleza vielelezo hivyo ni vya zaidi ya kesi 30 za dawa za kulevya za watuhumiwa wa ndani na nje ya nchi huku akieleza mbali na watuhumiwa kuhukumiwa pia baadhi ya mali zao zimetaifishwa na Serikali.
Naye kamishna wa sayansi na jinai kutoka mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya nchini Bi.Bertha Mamuya amebainisha kwamba uteketezaji wa dawa hizo hauna athari ndani ya jamii.