Emmanuel Lyimo Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la TFCG akifungua semina ya waandishi wa habari kuhusu masuala ya jinsia na utunzaji wa misitu inayofanyika kwenye hoteli ya Edema mjini Morogoro.
Mkufunzi wa mafunzo hayo Profesa John Jeckoniah kutoka Chuoa Kikuu cha Kilimo SUA mkoani Morogoro akitoa mada katika semina hiyo.
Picha mbalimbali zikionesha baadhi ya washiriki wa semina hiyo wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa na watoa mada.
Picha za pamoja mara baada ya kufunguliwa kwa semina hiyo.
…………………………………………….
Na. Suleiman Msuya, Morogoro
WAANDISHI wa habari nchini wameshauriwa kuandika habari za Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) kwa kuzingatia usawa wa kijinsia ili kuchochea maendeleo kwa jamii husika.
Ushauri huo umetolewa na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Profesa John Jeckoniah wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka kwa vyombo vya habari mbalimbali nchini.
Amesema mafunzo hayo jinsia ambayo yameamdaliwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Usimamizi wa Misitu ya Jamii Tanzania ((MJUMITA) yataweza kubadilisha uelewa wa waandishi wa habari nchini kwa kuandika habari zenye usawa na uwiano.
Prof.Jeckoniah iwapo waandishi wa habari wakijengewa uwezo katika eneo hilo wataweza kutoa habari zenye tija na kuchochea mabadiliko kwa jamii kwa ujumla.
Aidha amesema kuwa uwiano wa masuala ya kijinsia nchini bado upo chini hivyo njia sahihi ya kufanikiwa katika eneo hilo ni kuwajengea uwezo waandishi ili wawe na uwanja mpana katika kuripoti hasa kwenye USMJ.
“Katika hali ya maendeleo nchini uwiano wa kijinsia bado haupo vizuri pamoja na ukweli kuwa wanawake wanaweza kufikia rasilimali ila uamuzi wa mwisho kuhusu matumizi ya rasilimali inabakia kwa wanaume jambo ambalo linapaswa kupingwa na wadau wote,” ameeleza.
Vile vile amesema juhudi za kubadilisha jamii zinafanyika kwa kuwajengea uwezo wahusika wote ili kwenda kwa pamoja.
“Serikali imekuwa ikifanya jitihada kwa kuandaa sera, sheria na miongozo ila tatizo kubwa lipo ngazi ya chini za utekelezaji hivyo wanawake kuwa waathirika wakubwa na njia ya kutoka hapo ni waandishi kutumia nafasi zao kubadilisha,” amebainisha.
Mhadhiri huyo ametoa rai kwa wawakilishi wa wananchi kuzingatia masuala ya kijinsia katika mipango ya maendeleo ili kuchochea maendeleo.
“Viongozi wapya ambao wamepewa nafasi na wananchi wanapaswa kujikita katika kuelewa kwa kina namna ya dhana ya jinsia inavyoweza kuchochea maendeleo kwa jamii ikiwemo inayojihusisha na USM,” amesisitiza.
Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo amesema mafunzo hayo kwa waandishi wa habari kuhusu jinsia ni moja ya mkakati wao kwenye Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) ambao umechochea mabadiliko makubwa kwenye USM.
Hata hivyo amesema mikakati mingine ni kuchochea shughuli za maendeleo, kulinda mazingira, mawasiliano na uraghibishi, ushirikiano na wadau mbalimbali na kujenga taasisi imara yenye nguvu.
“Imani yetu ni kwamba kupitia mafunzo haya waandishi mtakuwa na uelewa mpana wa kuandika habari za jinsia hasa kwenye eneo la USMJ,” ameeleza.
Meneja Mradi wa TTCS, Charles Leonard ameongeza kuwas mradi huo ulijikita kuwainua wananchi kwa kuzingatia usawa wa kijinsia jambo ambalo limesaidia uwe unapokelewa vizuri katika maeneo mengi.
Leonard amesema awamu ya kwanza na ya pili wamefanikiwa kuwepo kwa matumizi bora ya ardhi kwenye hekta 130,000.
“Pia mradi umechochea uhifadhi wa misitu kwenye vijiji, kukuza uchumi wa wanavijiji na kijiji kwa ujumla na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,” ameeleza.
Lakini pia amesema kwa sasa wanatekeleza awamu ya tatu ya mradi ambao unajulikana kama Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Misitu (CoFoREST).
Meneja huyo amesema mradi wa CoFoREST utahusisha wilaya nyingi zaidi huku mkazo ukijikita kwenye kuwajengea uwezo watumishi na wataalam kutoka Serikalini ili watekeleze mradi wenyewe.