…………………………………………………………………………
Na John Walter-Hanang’
Mkuu wa wilaya ya Hanang’ Ghaibu Lingo ameweka jiwe la Msingi katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Bama, unaoendelea kujengwa kwenye shule hiyo iliyopo Kijiji cha Lamay mkoani Manyara.
Zaidi ya Shilingi Milioni 200 zinatarajiwa kutumika Mpaka kukamilika Kwa ukumbi huo ambao utakuwa unatumiwa na wanafunzi katika shughuli mbali mbali ikiwemo midahalo.
Pamoja na kuweka jiwe la Msingi Lingo alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya mahafali ya nane ya kuwaaga wahitimu wa kidato cha nne shuleni hapo ambapo aliwataka wazazi kuendelea kuwalinda watoto hao pindi watakapokuwa majumbani mwao wakisubiri matokeo yao.
Meneja wa shule hiyo Mheshimiwa Potrajia Baynith amesema lengo ni kuboresha zaidi mazingira kwa ajili ya kumpatia mwanafunzi elimu iliyo bora.
Amewaomba wazazi kuendelea kusimamia nidhamu ya watoto wao kama ilivyokuwa shuleni hapo huku akiwataka wanafunzi wanaohitimu kujilinda na vishawishi mbalimbali ili watimize ndoto walizonazo.
Amesema shule hiyo ina mazingira rafiki kwa ajili ya wanafunzi wa Kike na wa kiume hivyo wazazi na walezi wasisite kuwapeleka watoto wao katika shule hiyo.
Akizungumzia hali ya Taaluma Mkuu wa shule Eva Massawe, amesema imekuwa ya kutia moyo siku hadi siku kutokana na jitihada za walimu,wanafunzi, wazazi pamoja na wadau wengine wa Elimu.
Massawe amesema pamoja na yote hayo wanakabikliwa na changamoto ya Umeme licha ya kuahidiwa kuwa shule imeingia kwenye mpango wa kupatiwa huduma hiyo kupitia mradi wa usambazaji Umeme vijijini awamu ya tatu.
Mkuu wa wilaya Ghaibu Lingo ameahidi kushughulikia changamoto hiyo ili nishati hiyo ifike shuleni hapo wanafunzi waweze kujisomea hata nyakati za usiku.
Shule ya Sekondari Bama ilianza Januari 26,2011 ikiwa na wanafunzi saba ambapo mpaka kufikia mwaka 2020 ina jumla ya wanafunzi 315, kati ya hao 114 wanahitimu masomo ya kidato cha nne wavulana 36 na wasichana 78.