************************************
NA FARIDA SAIDY,MOROGORO
Joto la Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania linazidi kupamba moto ambapo taifa kwa ujumla linafanya uchaguzi wake wa tano tangu kuasisiwa kwa Demokrasia ya vyama vingi zaidi ya miongo miwili iliyopita.
Nchini Tanzania vyama vya siasa vimekamilisha michakato ya ndani ya kuwatafuta makada watakaoviwakilisha vyama vyao katika uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2020.
Kimbembe kipo pale kwenye mji wenye milima mingi yenye kuvutia wao wanaita milima ya Uruguru na si kwingine ni pale Morogoro Mjini kwa aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo Abdul-Aziz Mohamed Abood.
Sasa kuna chuma kingine ambacho kimeahidi kumpindua Bw.Abood kwenye Uchaguzi Mkuu upande wa Ubunge wa Jimbo hilo.
Ni mwanamama ambaye alikuwa Mbunge wa Viti maalumu katika miaka mitano kwasasa anapambania nafasi ya Ubunge kwenye Jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.
Ni Devotha Micha ambaye pia ndiye mgombea pekee wa Ubunge kwa upande wa wanawake Mkoa wa Morogoro.
Katika sera zake amewataja pia wanawake kuwa kipaumbele chake katika uchaguzi huo ambao unaenda kufanyika tarehe 28 mwezi wa Oktoba mwaka huu.
Devotha amesema katika kipindi cha miaka mitano akiwa kama mbunge wa viti maalumu amefanya mambo makubwa kwa wanawake wa mkoa wa Morogoro.
Amesema akiwa Bungeni alipata nafasi ya kuwasemea wanawake kero zao mbalimbali ikiwemo huduma za afya,maji,miundombinu ya barabara,ambapo katika kipindi hicho cha miaka mitano kunamabadiliko kadhaa yamefanyika katika vituo vya afya jambo ambalo limesaidia kupunguza vifo vya wakina mama na mtoto hususani vijijini.
Hata hivyo licha ya kuwa mtetezi wa wanawake wenzake Bungeni akiwa kama Mbunge wa viti maalumu, kwa sasa Devotha ameamua kugombea Ubunge kupitia chama chake kama mwanamke pekee ambaye anagombea katika jimbo la Morogoro Mjini na kuwataka wanawake kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa kampeni zake katika jimbo la Morogoro mjini, Devotha amewataka wanawake wa Morogoro kumchagua kwani yupo tayari kuwasemea kero zao endapo watampa ridhaa ya kuwa Mbunge wa jimbo .
Amesema atahakikisha swala la ajira kwa vijana na wanawake Morogoro Mjini linabaki kuwa historia, kwani atahakikisha vijana wananufaika katika viwanda vilivyopo na hata vile vilivyofungwa atahakikisha vinafanya kazi ili kuongeza ajira kwa wananchi wa jimbo hilo.
Aidha akiwa katika Kata ya Mkundi Devotha amewaahidi wanawake wa kata hiyo kuwa akiwa Mbunge wa hilo atahakikisha Kata ya Mkundi inapata maji safi na salama hali itakayowasidia wanawake kufanya shughuli za kiuchumi na kuachana na adha ya kutafuta maji umbali mrefu.
Hata hivyo Devotha amewataka wanawake kujitokeza katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi ya mtaa hadi Taifa kwani wanawake wanauwezo mkubwa katika uongozi.
“Tukisia kuna nafasi zimetangazwa sehemu yoyote nawaomba wanawake wenzangu tujitokeze kuomba nafasi hizo tusikae tu na kusema hatuwezi”.Alisema Devotha.
Pia Kwenye upande wa miundombinu mgombea huyo amesema kuna maeneo kama kata ya Tungi,Kihonda,Lokobe na maeneo mengine ambayo barabara zake za mtaa bado hazijawekewa rami hali inayopelekea wakati wa mvua wananchi kukosa barabara ya kupitishia magari yao, nazo zote atahakikisha zinapitika kwa nyakati zote iwe mvua ua jua.
Sambamba na yote devotha amewataka wananchi wa Mkoa wa Morogoro kijitokeza kwa wingi Tarehe 28 oktoba mwaka huu kwenda kutimiza takwa la kikatiba la kuwachagua Madiwani,Wabunge na Rais,ambapo zoezi hilo huo linatokea mala baada ya mika mitano.