Halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe iliyokutana Julai mosi 2019 katika ukumbi wa TURBO Njombe mjini, ilitoka na maazimio mbalimbali pamoja na kuipongeza Serikali mkoani humo kwa Utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika Miradi ya Afya, Barabara na Elimu.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Siasa na Uenezi wa chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe Ndg, Erasto Ngole, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake na kuongeza kuwa, kikao hicho kimeielekeza Serikali mkoani humo kuhakikisha Kasi ya Ujenzi wa Barabara ya Lami kutoka Njombe kwenda Ludewa inaongezeka.
Amesema chama kimeielekeza Serikali kuhakikisha Ujenzi wa Barabara ya kutoka Njombe kupitia Lupembe hadi Madeke unaanza maramoja, ili kuwapunguzia Wananchi wa maeneo hayo tatizo la usafiri hasa kipindi cha Masika.
Ameongoza kuwa Kikao kimeelekeza Mkuu wa mkoa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, wakutane na Wadau mbalimbali ili kujadili namna bora ya uendeshaji wa Kituo kipya cha Mabasi kilichopo eneo la Mjimwema Njombe mjini, kwa lengo la kujadili na kuondoa kero zilizopo katika kituo hicho.
Kuhusu Vitambulisho vya Wajasiriamali Ngole amesema kuwa Kikao kilimpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli, kwa ubunifu wa kuwasaidia Wajasiriamali kote nchini ili wasikutane na usumbufu katika Biashara zao.
Katibu huyo wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Njombe ameeleza kuwa Kikao kimebaini kuwa, baadhi ya Wadau mkoani Njombe hawana ufahamu wa kutosha juu ya Vitambulisho hivyo na Kikao kimeielekeza Serikali kutoa waraka utakao ainisha kundi linalostahili kupata vitambulisho hivyo.
“Tukiwa na waraka utasaidia Watendaji wa Serikali kuwa na uelewa wa pamoja juu ya utekelezaji wa swala hili, ili lengo la Taifa lisipotoshwe na watu wachache, pia kikao kimekubaliana kuwa wana siasa wote wanatakiwa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza hoja hii muhimu” Ameeleza Erasto Ngole.
Aidha kuhusu Taarifa ya Viongozi na Wanachama kutoka vyama vingine vya siasa wanaohamia chama cha mapinduzi mkoa wa Njombe, Ndg, Erasto Ngole amesema kuwa Hadi sasa chama kimewapokea Viongozi na Wanachama 237 kutoka vyama vya upinzani kuanzia ngazi ya Vijiji hadi mkoa.
“CCM inaamini kuwa ifikapo October 2019 wale wote waliokuwa wanaipinga CCM, watakuwa wanajiunga na chama hiki kutokana na uelekeo sahihi wa chama na Serikali wa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi na kutatua kero za Watu” Erasto Ngole.
Akiendelea kutoa Taarifa kwa vyombo vya Habari Ngole amesema, Kikao cha Halmashauri kuu ya CCM mkoa kilipongeza maendeleo ya zoezi la kusajili Wanachama kupitia mfumo mpya wa Kielectronic linaloendelea katika wilaya zote za mkoa wa Njombe.
Kufuatia Changamoto ya huduma ya Maji katika baadhi ya maeneo ya Miji ya Njombe, Makambako na Ilembula, kikao chini ya Mwenyekiti Mzee Jassel Mwamwala, kiliitaka Serikali kuharakisha ukamilishaji wa Miradi katika maeneo hayo pamoja na huduma ya Umeme wa REA katika Wilaya ya Wanging’ombe.
Katika hatua nyingine Katibu wa siasa na uenezi wa CCM mkoa wa Njombe amesema kuwa chama kinaitambua na kuithamini Sekta ya michezo, hivyo kikao kimeielekeza Serikali mkoani Njombe kuiboresha Sekta hiyo kwakuwa mkoa bado upo nyuma katika suala zima la michezo.
*Imetolewa na Ofisi ya Siasa na Uenezi CCM, mkoa wa Njombe.*