Na.John Bukuku,Tanga
MGOMBEA urais wa CCM Dkt.John Magufuli ameendelea kuchanja mbuga kwa kufanya Kampeni zake katika wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga huku akiendelea kuomba ridhaa ya wana CCM, na wananchi kumchagua kuwa Rais na kuchagua wabunge na madiwani wa CCM.
Akiwa katika Mkutano huo,Dkt.Magufuli amewaeleza wananchi wa Korogwe mkoani Tanga jinsi ya karatasi ya mfano ya mpiga kura inavyoonekana na kwa vipi wataweza kumpigia kura ili ashinde kwa kishindo.
Dkt.Magufuli amewakumbusha wananchi kuwa zimebaki siku nane kufanyika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu hivyo huu ndo mfano wa karatasi zitakazokuwa.
Dkt.Magufuli ameeleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) tayaru imetoa mfano wa karatasi ya fomu ya kupigia kura na katika fomu hiyo inaonesha Chama Cha Mapinduzi ndio namba moja kwenye fomu na linaanza jina la Mgobea mwenza Samia Suluhu Hassan na linafuata jina la Dk.John Pombe Magufuli na mbele ya majina hayo kuna kiboksi cha kuweka alama ya tiki.
“Yaani ikiingia kwenye chumba cha kupigia kura ukishachukua fomu hiyo utaona nimevaa miwani na kichwani nina kaupara, hivyo nenda katika kiboksi weka alama ya tiki, hakikisha hauvuki chini ya mstari na baada ya hapo chukua kura karatasi yako ya kura weka katika boksi.Usihangaike na wengine walipo katika fomu hiyo ya kupiga kura kwani hawatuhusu,”amesema.
Aidha Dk.Magufuli amewataka wananchi kujitokeza siku ya kupiga kura na itakuwa siku ya mapumziko kitaifa ili wananchi wakapige kura na baada ya kupiga kura warudi nyumbani kusubiri matokeo.