Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Mtibwa Sugar imezinduka baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Namungo FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa CCM Gairo mkoani Morogoro.
Ushindi huo unaokuja siku moja baada ya timu hiyo kuachana na kocha wake Mkuu, Zubery Katwila umetokana na bao pekee la kiungo Salum Kihimbwa kwa penalti dakika ya 76.
Na kwa ushindi huo leo chini ya kocha wa Muda, Vincent Barnabas mchezaji wa zamani wa Mtibwa pia kama Katwila, timu hiyo inafikisha point inane baada ya kucheza mechi saba na kujiinua kutoka nafasi ya 15 hadi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakati Namungo FC inabaki nafasi ya nane na pointi zake tisa baada ya mechi saba.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Coastal Union imeichapa Biashara United 3-0, mabao ya Hamad Rajab dakika ya 32 na Raizin Hafidh dakika ya 45 na 61 Uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
Polisi Tanzania imeshindwa kutamba katika uwanja wa nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya kufungana 1-1 na vijana wa Gwambina FC .
Bao la Jabir Aziz Stima dakika ya 85 kwa penalti limeinusuru JKT Tanzania kulala mbele ya Polisi Tanzania iliyotangulia kwa bao la Jumanne Elfadhili dakika ya 21 baada ya timu hizo kutoa sare ya 1-1 Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
Ligi Kuu itaendelea kwa mechi nyingine nne kesho, ikiwemo vinara, Azam FC kuwa wageni wa Ihefu SC Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya wakati Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa KMC Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, mechi zote zikanzia Saa 8:00 mchana.
Baadaye Saa 10:00 jioni, Mwadui FC wataikaribisha Mbeya City Uwanja wa Mwadui Complex, Kishapu mkoani Shinyanga na Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Dodoma Jiji FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.