Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi akisoma taarifa fupi ya hospitali, kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Bi. Ziada Sellah, kushoto ni Afisa Muuguzi kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto BI. Jamila Hamidu.
Bi. Ziada Sellah akizungumza na wauguzi alipotembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila hii leo.
Wauguzi na wakunga wakimsikiliza Mkurugenzi wa Uuguzi na Ukunga Tanzania mara baada ya kutembelea hospitalini leo kwa lengo la kujionea utendaji kazi na kuwasikiliza.
Muuguzi wa Hospitali ya Mloganzila Bw. Wilson Fungameza akimkabidhi Mkurugenzi wa Uuguzi na Ukunga kitabu alichokiandika ambacho kinaelezea kazi za wauguzi na wakunga.
Baadhi ya wauguzi na wakunga wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Uuguzi na ukunga Tanzania Bi.Ziada Sellah pamoja na ujumbe wake .
…………………………………………………………………………
Wauguzi na wakunga watakiwa kujiendeleza kitaaluma ili kuongeza maarifa zaidi na kuwa na ujuzi mpana wa kuhudumia wagonjwa.
Kauli hiyo imetolewa Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Bi. Ziada Sellah Bi. Ziada Sellah wakati akizungumza na wauguzi na wakunga wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila katika ziara yake ya kikazi ya siku moja hospitalini hapo.
Bi. Sellah ameeleza kuwa teknolojia inakuwa kwa kasi, ni wazi kuwa mambo mengi yanabadilika hivyo wauguzi na wakunga hawanabudi kujiendeleza zaidi ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknoloji.
“Nawashauri muongeze taaluma zaidi ili kuinua kiwango cha huduma za uuguzi na ukunga pamoja na kufanya tafiti ambazo zitaweza kutangaza taaluma yetu na kuonesha kazi zinazofanywa na wauguzi hasa ikizingatiwa kwamba asilimia 80 ya huduma zinazotolewa hospitalini wauguzi na wakunga wanamchango mkubwa. amesema Bi. Sellah”.
Aidha amewakumbusha wauguzi na wakunga kufuata taratibu na miongozo ya utumishi wa Umma na kuzingatia matumizi sahihi ya simu kwa kufuatilia vitu vya msingi na vyenye tija kwa taaluma yao na taifa kwa ujumla.
“Ninapenda kuwasihi mtumie simu kwa kujiongezea maarifa ikiwemo kutangaza shughuli za uuguzi na ukunga mnazozifanya ili kuleta matokeo chanya ili jamii iendelee kuthamini na kutambua mchango wenu’’amesisitiza Bi. Sellah.
Pia Bi. Sellah ametumia fursa hiyo kumpongeza muuguzi wa MNH-Mloganzila Bw. Wilson Fungameza kwa kutengeneza mashine rahisi (CPAP) ambayo inamsaidia kupumua mtoto mwenye matatizo ya upumuaji.
Kwa upande wake Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema huduma za kiuguzi zimeendelea kuimarika katika Hospitali ya Mloganzila hatua ambayo inaongeza idadi ya wagonjwa.
“Tunahudumia wagonjwa takribani 750 kwa siku idadi hii inajumuisha wagonjwa wa ndani na wa nje’’ amesema Dkt. Magandi.
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila ina jumla ya vitanda 608 ambapo kati yake vitanda 31 vya ICU, 12 kusafisha damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo, vitanda/vyumba 27 vya watu mashuhuri, 10 kwa ajili ya upandikizaji uloto (bone marrow transplant), 24 vya huduma za magonjwa ya dharura.