Mgombea ubunge wa Jimbo la Kibamba kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Mhe.Issa Mtemvu akimuombea kura Rais Dk.John Pombe Magufuli katika mkutano uliofanyika viwanja vya Barafu Mburahati Jijini Dar es Salaam.
Rais Dk. John Pombe Magufuli akiwaapisha wagombea wa Udiwani kupitia Chama cha Mapinduzi CCM wakati akiwaombea kura kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Jimbo la Ubungo katika viwanja vya Barafu Mburahati jijini Dar es salaam leo Jumanne Oktoba 13 ,2020.
**************************************
NA EMMANUEL MBATILO
Mgombea Ubunge Jimbo la Kibamba Mhe.Issa Mtemvu amemwagia sifa Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli kwa maendeleo ambayo ameyafanya katika jimbo la Kibamba ikiwemo upanuzi wa barabara katika maeneo mbalimba pamoja na miradi mikubwa ya maji.
Akizungumza katika Kampeni za Mhe.Rais Magufuli katika Jimbo la Ubungo Mhe.Mtemvu amesema miradi mikubwa miwili ya maji katika maeneo mbalimbali yakiwemo maeneo ya Tegeta, Goba, Mbezi na maeneo mengine ni mojawapo ya mendeleo makubwa kwa wananchi wa jimbo la Kibamba.
“Upo mtandao wa Kilomita 315 ambao umeendelea kutandazwa kuanzia Mbezi Luis hadi Kiluvya Madukani, Mhe.Rais kwa unyenyekevu mkubwa na mapenzi makubwa kwa watu wa Kibamba tunakushukuru sana”. Amesema Mhe.Mtemvu.
Aidha Mhe.Mtemvu amesema kuwa kutokana na uhaba wa zahanati amemshukuru Mhe.Rais kuwaletea hospitali ya Wilaya na mpaka sasa hospitali hiyo inaigharimu zaidi ya Bilioni 1.8 lakini tayari amewawekea fedha na matumizi yao ni zaidi ya Milioni 603 mpaka sasa.
Hata hivyo Mhe.Mtemvu amesema kuwa Sera aliyoileta Mhe.Dkt.Magufuli ya elimu bila malipo imewasaidia wananchi wa Kibamba kwasababu tayari kunaongezeko la kuandikisha watoto darasa la kwanza, zaidi ya asilimia 16 ambao ni watoto 8118 tayari wamesajiliwa kuanza darasa la kwanza.