Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)
Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Serikali imetangaza kiama kwa wanaochelewesha mbolea kuwafikia wakulima kwa wakati kwani kuchelewa kwa mbolea ni miongoni mwa sababu zinazopunguza uzalishaji wa mazao mbalimbali ya wakulima nchini.
Mbolea kutofika kwa wakulima kwa wakati ni wazi kuwa Taasisi iliyopewa jukumu la kusimamia na kudhibiti mbolea ya TFRA imeshindwa kufanya kazi yake kwa ufasaha hivyo ikibainika kuchelewa kwa mbolea pasina sababu za msingi watendaji hao watachukuliwa hatua za kisheria.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametoa kauli hiyo ya onyo leo tarehe 4 Julai 2019 Jijini Dar es salaam wakati akizungumza kwenye kikao kazi na wafanyakazi wa Taasisi ya udhibiti wa mbolea Tanzania (TFRA).
Alisema kuwa mbolea inayohitajika kwa wakulima ni Lazima ipatikane kwa wakati katika maeneo ya kilimo. “Kupatikana kwa wakati maana yake ni kwamba kila mtu anapoishi anapaswa kuipata kirahisi kupitia maduka au masoko” Alisema
Aliongeza kuwa kazi ya Taasisi ya udhibiti wa mbolea Tanzania ni kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima sio kusalia Jijini Dar es salaam ilihali wakulima wapo mikoa yote Tanzania na endapo mbolea ikikosekana kwa wakulima watendaji wa TFRA watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Kadhalika alisema kuwa kupatikana pekee kwa mbolea kwa wakulima ni jambo moja lakini muhimu ni kuwa na bei nafuu ambazo wakulima wataweza kuzimudu.
“Sasa hivi kuna malalamiko mengi kwa wakulima kuwa mbolea zinauzwa bei ya juu hivyo wameshindwa kuzimudu, haiwezekani mbolea itoke Ulaya ikiwa na bei nafuu lakini kumfikia mkulima inakuwa na bei ghali, hapo ni wazi kuwa TFRA hamjafanya kazi yenu sawasawa” Alikaririwa Mhe
Hasunga
Hasunga
Alisema kuwa endapo TFRA itatekeleza majukumu yake ipasavyo mbolea itapungua bei na wakulima watanufaika na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Tanzania.
“Na kama tatizo la gharama linaongezeka kutokana na usafirishaji kuna sababu gani za kutumia magari kusafirisha wakati kuna usafiri muhimu wa reli (TRC) ambapo mawakala wangepakua na kusambaza mizigo hiyo baada ya kufika katika maeneo mbalimbali inapoishia reli” Alisema
Hata hivyo amesisitiza kuwa serikali imeanzisha mchakato wa kupitia mbolea kote nchini ili uagizaji wa mbolea iweze kuagizwa itakayoendana na uwezo wa udongo.