Mfanyabiashara wa Matunda wa Kata ya Ihanja Robert, akizungumzia umuhimu wa vitambulisho hivyo.
Mama Lishe Pili Juma wa Puma, akizungumzia umuhimu wa vitambulisho hivyo.
Rehem Said, Mfanyabiashara wa Nkhunikana akizungumzia umuhimu wa vitambulisho hivyo na alimpa pongezi nyingi Rais Magufuli kwa kutoa vitambulisho hivyo.
Gaudensia Paul mkazi wa Kideka, akizungumzia vitambulisho hivyo.
Baraka Paul kutoka Kijiji cha Kideka alisema vitambulisho vimepanua wigo wa kufanya biashara.
Na Dotto Mwaibale, Ikungi
WAFANYABIASHARA wadogo katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida , wamesema watu wanao vibeza vitambulisho vya wajasiriamali hawana uzalendo wa nchi yetu na kuwa wanawashangaa wanaopotosha umuhimu wa vitambulisho hivyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wilayani hapa wananchi hao walisema wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, kwa kuwapa vitambulisho hivyo ambavyo vimewafanya wawe huru na kuwa pungumzia gharama kubwa iliyotokana na ulipaji wa ushuru mkubwa.
Akizungumzia vitambulisho hivyo Mfanyabiashara wa Matunda wa Kata ya Ihanja aliyejitambulisha kwa jina moja la Robert alisema hivi sasa wapo huru baada ya kuanza kutumia vitambulisho hivyo.
“Sasa hivi adha ya kufukuzana na mgambo walikuwa wakipita kudai fedha za ushuru haipo tena na zile Sh. 200 tulizo kuwa tukilipa kila siku ambapo kwa mwezi ilikuwa ni Sh.60,000 hazipo kwani tukilipa Sh. 20,000 hakuna malipo mengine kwa mwaka mzima” alisema Robert.
Mama Lishe Pili Juma wa Puma alisema tangu aanze kutumia vitambulisho hivyo amekuwa huru na amewaomba wafanyabiashara wenzake kutodanganyika na wanaodai vitambulisho hivyo kuwa havina tija.
Rehema Said Mfanyabiashara wa Nkhunikana alisema anampa pongezi nyingi Rais Magufuli kwa kutoa vitambulisho hivyo ambavyo vimewafanya waheshimike na kuwa zawadi pekee ni kumpa kura nyingi ifikapo Oktoba 28.
Mfanyabiashara Martina Michael wa Kijiji cha Nkhunikana alisema Sh.500 waliokuwa wakilipa kila siku sawa na Sh.150,000 kwa mwezi zilikuwa ni nyingi ukilinganisha na Sh.20,000 wanayoitoa sasa kwa mwezi na kuwa wanafurahia kufanya biashara.
Kwa upande wake Gaudensia Paul mkazi wa Kideka, aliomba kiasi hicho cha Sh.20,000 wanacho kitoa kipunguzwe na wale wanaobeza vitambulisho hivyo wapuuzwe na kuwa hawana uzalendo wa nchi yetu.
Baraka Paul Mfanyabiashara kutoka Kijiji cha Kideka alisema vitambulisho hivyo vimepanua wigo wa kufanya biashara kwani hivi sasa wanapeleka biashara zao hadi mikoa mingine bila ya kubugudhiwa.
Wafanyabiashara hao walimpongeza Rais Magufuli kwa kuwaletea vitambulisho hivyo kwa Sh. 20,000 tu kwa mwaka na kuondokana na changamoto za kukimbizana na mgambo na kuwa sasa biashara zao zimeimarika zaidi na kipato chao kimeongezeka huku baadhi yao wakifanikiwa kununua ardhi, kusomesha watoto na kujenga nyumba.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo alisema kwa mwaka jana vitambulisho 7,800 vilitolewa kwa wafanyabiashara hao na kuwa mwaka huu vimetolewa 3,600 sawa na asilimia 58 na bado vinaendelea kutolewa.
“Vitambulisho hivi vimesaidia kuongeza mapato ya wilaya yetu kwani hapo awali fedha nyingi zilizokuwa zikipatikana kutokana na ushuru ziliishia mikononi mwa wajanja.” alisema Mpogolo.
Mpogolo alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Dkt.John Magufuli kwa kuwa na maono makubwa ya kuanzisha mpango huo ambao umekuwa ni mkombozi kwa wafanyabiashara ndogondogo kote nchini.
Hivi karibuni baadhi ya wanasiasa wakiwa kwenye kampeni waliibuka na kuanza kupotosha umma kuhusu vitambulisho hivyo vya wajasiriamali ‘maarufu kama vya wamachinga’ kuwa haviwanufaishi na badala yake wanaibiwa, kauli ambayo Rais John Magufuli ambaye ni Mgombea wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliwataka wafanyabiashara hao kuwapuuza badala yake waunge juhudi za serikali za kuwaletea maendeleo.