******************************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imeazimia kuhakikisha barabara ya lami ya kuelekea mtaa wa Kairo inawekewa madaraja madogo ili maji yapate upenyo mkubwa wa kupita na kuepusha mafuriko wakati wa mvua.
Mwenyekiti wa mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani Adam Kobelo aliyasema hayo juzi kwenye kikao cha mamlaka ya mji huo.
Kobelo alisema shughuli hiyo itafanyika kwa wakati huu ambapo hakuna mvua ili madhara ya mafuriko yasitokee tena pindi mvua kubwa zikinyesha.
Alisema alishazungumza na wakala wa barabara nchini (Tanroads) mkoani Manyara kwa ajili ya kifanikisha ujenzi wa madaraja hayo madogo ya kupitisha maji.
Alisema wataalamu wa Tanroads mkoani Manyara walipita kwenye barabara hiyo na kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
“Sisi kama viongozi tulisimama kwenye nafasi yetu na kifanikisha kuonana na viongozi wa Tanroads ili barabara hiyo ifanyiwe ukarabati,” alisema Kobelo.
Awali, Mwenyekiti wa mtaa wa Kairo, Gadi Msuya alisema kipindi Cha mafuriko wananchi wengi nyumba zao zilibomoka kutokana na barabara hiyo kushindwa kupitisha maji kwa wingi.
Msuya alisema endapo suala hilo litapatiwa ufumbuzi itakuwa nafuu kwa wananchi kwani kipindi cha mvua kikifika maji yatakuwa na sehemu ya kupitia tofauti na awali.
Mwenyekiti wa mtaa wa Tanesco, Justin Abraham alisema kero hiyo itafikia kikomo endapo utekelezaji wake unafanyika kwani wananchi wengi wameathirika na mafuriko kutokana na maji kukosa sehemu ya kupitia.
“Wananchi wa Mireeani hawatatuelewa kama barabara hiyo haitawekwa madaraja madogo yatakayoruhusu maji kupita kwa wingi hasa kipindi cha mafuriko,” alisema.