Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu akizungumza na waasisi wa Umoja wa Jumuiya za Wanawake wa nchi huru za Afrika (PAWO) jijini Dar es salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto – akiwa katika picha ya pamoja na waasisi wa Umoja wa Jumuiya za Wanawake wa nchi huru za Afrika (PAWO) jijini Dar es salaam
Mwenyekiti wa Umoja wa Jumuiya za Wanawake wa nchi huru za Afrika (PAWO) Leah Lupembe akimueleza jambo Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu wakati wa mkutano na waasisi wa Umoja huo Jijini Dar es salaam.
Picha zote na kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Afya – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amewataka waasisi wa Jumuiya za wanawake wa nchi huru za Afrika PAWO kuendelea na mapambano ya kuwakomboa wanawake kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Akizungumza na waasisi hao jijini Dar es salaam Dkt. Jingu amesema PAWO imetoa mchango mkubwa katika bara la Afrika wakati wa harakati za kuondokana na ubaguzi wa rangi na ukandamizaji wa wakoloni lakini bado mapambano yanaendelea ambayo ni kujikomboa kiuchumi katika nchi na mtu mmoja mmoja.
Ameongeza pia, Serikali kupitia Wizara ya Afya – Idara Kuu ya Maendeleo ya jamii imeweka kipaumbele suala zima la kuwakomboa wanawake kiuchumi kwa kutambua kuwa, mwanamke akiwezeshwa kiuchumi ataweza kujitegemea kwa mambo mengi hivyo kuepukana na unyanyasaji unaotokana na uchumi duni.
“Katika shughuli zetu zote tumeweka suala la kuwawezesha wanawake kiuchumi kuwa kipaumbele, tunafanya hivyo kwa sababu tunajua mwanake akiwezeshwa kiuchumi mambo mengine yote yanaweza kufunguka”amesema Jingu.
Katibu wa Umoja huo hapa nchini Marie Shaba amesema, tangu kuanzishwa kwake umoja huo Pamoja na shughuli nyingi walizofanya waasisi, wameamua kuendelea kupambana kwa kufanya kampeni kuibua mambo ambayo yatafanya jamii iweze kubadili fikra na tabia katika ngazi zote ikiwemo mila na desturi.
Naye mwanasheria kutoka Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Charles Mpaka amewashauri waasisi hao kufuata sheria na taratibu za usajili wa mashirika na kuwa, Ofisi ya Msajili ipo tayari kuwapa ushirikiano.
Umoja huo ulianzishwa mwaka 1962 kwa lengo la kuwaunganisha wanawake wa nchi za Afrika ili kutoa msukumo wa kushirikishwa kiuchumi na kijamii ambapo kwa sasa umoja huo unaingia hatua ya kuwa shirika lisilo la Kiserikali kuendeleza majukumu yake.