Ofisi za Jeshi la Polisi mkoa wa Katavi
Baadhi ya watoto wakicheza katika moja ya mtaa wa Manispaa ya Mpanda
……………………………………………………………………………..
Na Zillipa Joseph, Katavi
Imeelezwa kuwa umaskini katika ngazi ya kaya ni sehemu mojawapo inayopelekea matukio ya ukatili wa kingono na kimwili dhidi ya watoto kuendelea kuripotiwa mkoani Katavi
Akizungumza na Full shangwe blog afisa wa Polisi kutoka dawati la Jinsia la Polisi mkoa wa Katavi Bi. Clara Ndyamkana amesema matukio hayo wakati mwingine yanafanywa na watu wa karibu kabisa na watoto wanaoathirika
Ameeleza kuwa watoto wanaofanyiwa vitendo hivyo huathirika kisaikolojia na hivyo kuathiri ukuaji wa mtoto
“Makosa mengi yanayoongoza kuripotiwa kwa kipindi cha miezi sita iliyopita ni ubakaji, ulawiti na shambulio la mwili” alisema
Bi Ndyamkana ameendelea kueleza kuwa umaskini unasababishwa na wazazi kutokufuata uzazi wa mpango hali inayopelekea kuwa na watoto wengi huku kukiwa hakuna shughuli maalum ya kujiongezea kipato
Amesema hali hiyo inapelekea watoto kuachiwa wakizurura hovyo na wakati mwingine kutekwa na kubakwa katika maeneo mbalimbali watoto waliyokwenda kucheza
“Imani za kishirikina katika mkoa wa Katavi ni sababu nyingine ya kubakwa au kulawitiwa kwa watoto au kutekwa kwa watoto” alisema
Ameeleza kuwa hali hiyo inasababishwa na uchimbaji wa madini ya dhahabu ambapo wahusika wamekuwa wakifuata masharti ya waganga wa kienyeji
Aidha ametoa wito kwa wazazi kuwa makini kulinda watoto wao ili kuwalinda dhidi ya watu waovu
Kuhusu vitendo vya utekaji wa watoto amesema kwa kipindi cha miezi sita hakuna ripoti ya kutekwa kwa watoto wadogo iliyotolewa
Bi. Maimuna Kundali ni mkazi wa Kawajense katika Manispaa ya Mpanda, ametoa wito kwa wazazi kuwa tabia ya kuchunguza watoto na hata kuwafuatilia pindi wanapowatuma dukani
Kama unaona uvivu kwenda mwenyewe mtume mtoto lakini simama eneo ambalo unaliona duka hiyo itakuwa rahisi kuona nani anamsemesha mtoto wako” alisema Kundali
Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera amewataka wazazi kuendelea kuwalinda watoto ili wasipate madhara ambayo yangeweza kuzuilika
“Wazazi waendelee kuwalinda watoto wao hasa wa chini ya umri wa miaka saba hasa wakati huu ambapo tuko katika kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu” alisema Homera
Kipindi cha miezi sita iliyopita kuliripotiwa matukio mawili ya utekaji wa watoto wenye umri ya chini ya miaka sita katika maeneo tofauti hali iliyopelekea mkuu huyo wa mkoa kutoa amri ya kutotuma watoto madukani hasa nyakati za usiku