Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Michael Mtenjele (kushoto), akizungumza na Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo kabla ya kuanza ziara ya kazi yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi husika,
Baadhi ya wanafunzi wakiwa katika foleni kuingia chumba cha Daktari katika Zahanati ya Kijiji cha Kyenda iliyoko wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera. Taswira hii ilichukuliwa Septemba 28, 2020 wakati wa ziara ya Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo (pichani), kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo. Zahanati hii imejengwa kupitia Mradi husika.
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikikagua tanki la maji linalojengwa katika Kitongoji cha Ngome, Kijiji cha Kasulo, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera kupitia Mradi huo, Septemba 28, 2020. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo.
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikikagua nyumba ya kuishi walimu katika Shule ya Sekondari Mumiterama, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera iliyojengwa kupitia Mradi huo. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo.
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikikagua ujenzi wa Tanki la Maji, eneo la Rusumo, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo .
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikikagua Jengo la Madarasa katika Shule ya Sekondari Mumiterama, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera iliyojengwa kupitia Mradi huo. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo.
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo ikizungumza na wanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Rusumo iliyoko kijiji cha Kyenda, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo Septemba 28, 2020 ambapo Shule hiyo imenufaika kwa kujengewa vyumba vya madarasa na vyoo vya wanafunzi.
Sehemu ya majengo ya Kituo cha Afya Rusumo, kilichoko wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera, kinachojengwa kupitia Mradi wa Umeme wa Rusumo unaotekelezwa wilayani humo. Taswira hii ilichukuliwa Septemba 28, 2020 wakati wa ziara ya Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi huo, kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi husika.
Baadhi ya wajumbe wa Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo wakijadiliana jambo nje ya Zahanati ya Kijiji cha Kyenda, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera baada ya kufanya ukaguzi katika Zahanati hiyo wakiwa katika ziara ya kazi, Septemba 28, 2020. Kutoka kulia ni Kiongozi wa Msafara, Mhandisi Innocent Luoga ambaye ni Kaimu Kamishna kutoka Wizara ya Nishati na Mjumbe wa Bodi ya Mradi huo, Mhandisi Salum Inegeja kutoka Wizara ya Nishati na Mhandisi Costa Rubagumya kutoka TANESCO ambao ni wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mradi.
Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi wa Umeme wa Rusumo wakijadiliana jambo baada ya kukagua vyoo vya wanafunzi katika Shule ya Sekondari Mumiterama, wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera vilivyojengwa kupitia Mradi huo. Timu hiyo ilikuwa katika ziara kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa na Mradi huo.
…………………………………………………………………………..
Veronica Simba – Ngara
Serikali imeeleza kuwa Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera, unaotekelezwa Rusumo wilayani Ngara, una manufaa mtambuka kwa Watanzania.
Hayo yalielezwa jana, Septemba 28, 2020 na Timu ya Serikali kutoka Tanzania inayosimamia Mradi huo ikihusisha Wakurugenzi wa Bodi na Kamati ya Ufundi, wakiwa katika ziara ya kazi yenye lengo la kukagua miradi mbalimbali ya kijamii inayotekelezwa kupitia Mradi husika.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Kiongozi wa Timu hiyo, Mhandisi Innocent Luoga ambaye ni Mjumbe wa Bodi wa Kamati husika, alisema mbali na umeme, Mradi huo utawanufaisha Watanzania kupitia miradi mbalimbali ya kijamii ambayo alisema iko katika hatua nzuri za utekelezaji.
Mhandisi Luoga ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Umeme kutoka Wizara ya Nishati alieleza kuwa miradi ya kijamii inayotekelezwa ni pamoja na inayohusu sekta za afya, elimu, maji, mifugo na kilimo.
Akizungumzia lengo la Timu hiyo ya Serikali kutembelea miradi ya kijamii inayoendelea kutekelezwa, Mhandisi Luoga alisema ni kujionea hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wake, kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi ili kuwezesha miradi hiyo kukamilika kwa wakati.
“Tumetembelea shule za msingi na sekondari, zahanati, vituo vya afya na miradi ya maji ambayo yote inayotekelezwa hapa Ngara na tumejiridhisha kuwa kwa sehemu kubwa imefkia hatua nzuri na baadhi yake imekamilika.”
Hata hivyo, alieleza kuwa Timu yake imebaini changamoto ya baadhi ya miradi kusuasua hususan Mradi wa Maji unaotekelezwa Rusumo ambao umechelewa kutokana na kukosekana vibali vya ujenzi.
Alisema yeyé na wenzake wametatua changamoto husika kwa kuelekeza vibali hivyo vipatikane haraka ili Mkandarasi aanze kazi na kukamilisha Mradi kwa wakati.
Aidha, kwa miradi mingine inayosuasua inayohusu majengo ya shule na vituo vya afya, Timu iliwataka wakandarasi husika kukamilisha kazi kwa wakati, kuzingatia viwango na ubora.
Kuhusu manufaa ya umeme, Mhandisi Luoga alieleza kuwa Mradi wa Rusumo utakapokamilika utazalisha megawati 80 ambazo zitagawanywa kwa nchi tatu zinazohusika ambazo ni Tanzania, Rwanda na Burundi kwa kila moja kupata megawati 27.
Alisema kuwa kwa upande wa Tanzania, Mradi utasaidia kuongeza umeme katika gridi ya Taifa pamoja na kuboresha hali ya upatikanaji nishati hiyo katika Mkoa wa Kagera.
“Kama alivyoelekeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli, kuwa Mkoa wa Kagera uingizwe katika gridi ya Taifa, hivyo kukamilika kwa Mradi wa Rusumo kutawezesha hilo.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Michael Mtenjele, akizungumza na Timu hiyo ofisini kwake kabla ya kuanza ziara, alipongeza kazi nzuri inayoendelea kufanyika ambayo alisema imeleta manufaa makubwa kwa wananchi wake.
“Miundombinu ambayo imejengwa ni ya kipekee. Hatukuzoea kuona Shule za Msingi zinakuwa na Jengo la Utawala lakini kupitia Mradi huu hilo limefanyika na kwakweli inapendeza sana,” alifafanua.
Naye Mratibu wa Miradi ya Maendeleo ngazi ya Wilaya, Herman Hume alieleza kuwa miradi hiyo ya kijamii inayoendelea kutekelezwa wilayani Ngara ilitengewa fedha kiasi cha dola milioni tano za Marekani ambazo ni sawa na takribani shilingi bilioni 12 za Tanzania.
Wengine wanaoshiriki katika ziara hiyo itakayoendelea kwa siku mbili nyingine ni Mhandisi Salum Inegeja kutoka Wizara ya Nishati na Mhandisi Costa Rubagumya kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Mradi wa Rusumo.
Pia, Timu imefuatana na Mhandisi Patrick Lwesya, Meneja Mradi wa Rusumo, Gaspar Mashingia, Afisa Mwandamizi, Jamii, Maendeleo na Uhamaji Makazi pamoja na Maafisa kadhaa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ngara.