……………………………………………………………………………
Kiasi cha shilingi milioni 103 imekopeshwa kwa Vikundi vya wajasiriamali wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu kwa kata ya Buzuruga kwaajili ya kuendeleza shughuli walizonazo za uzalishaji mali na kujiongezea kipato ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Hayo yamebainishwa na mgombea ubunge wa jimbo la Ilemela kupitia chama cha mapinduzi Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa kata hiyo waliojitokeza katika mkutano wake wa kampeni kwaajili ya kuomba kuchaguliwa tena kuongoza jimbo hilo ambapo amesema kuwa kwa awamu iliyopita kata hiyo imenufaika na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya afya kwa kupanua kituo cha afya Buzuruga ambapo zaidi ya milioni 400 imetumika kujenga jengo la kuhifadhia maiti, jengo la maabara, jengo la wagonjwa wa nje, nyumba ya watumishi, ujenzi wa miundombinu ya barabara, ujenzi wa madarasa na uboreshaji wa sekta ya elimu ikiwemo kutoa elimu bila malipo sanjari na kutoa mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali
‘ Tumeingia katika uchumi wa kati miaka mitano kabla ya lilivyokuwa kusudio, Lakini katika hilo na nyingi wajasiriamali wadogo mchango wenu upo, Serikali ya Dkt Magufuli imetoa mikopo jitokezeni kukopa ‘ Alisema
Aidha Dkt Mabula ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya tano imeendelea kuhakikisha dawa zinapatikana na kuboresha huduma maalumu kwa wazee ambapo kwa wilaya ya Ilemela dawa zinapatikana kwa zaidi ya asilimia tisini huku akiahidi kushirikiana na wananchi wa mtaa wa Nyambiti kuanzisha Zahanati mpya itakayotoa huduma kwa wananchi wa eneo hilo.
Akimkaribisha mgombea huyo, Kampeni meneja Ndugu Kazungu Safari Idebe amewaasa wananchi wa kata hiyo kusikiliza Sera za wagombea na kufanya maamuzi sahihi kwa mustakabali wa maisha yao huku akisisitiza kutorudia makosa kwa kuchagua diwani asiejali wananchi anaowaongoza.
Nae mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Nelson Mesha mbali na kuwashukuru wananchi hao kwa kumuamini mgombea uraisi na ubunge wa chama chake katika uchaguzi wa mwaka 2015 akawaomba kutorudia makosa kwa kuchagua diwani wa upinzani kwani kufanya hivyo kutawacheleweshea maendeleo.