MKurugenzi Msaidizi Menejimenti ya Rasilimali Watu Wizara ya Maji Ingrid Sanda akimtwisha mama ndoo ya maji wakati wa ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Manyara
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa miundombinu ya maji mkoani Manyara
Wataalam wa kutoka wizara ya maji wakikagua kisima cha maji katika mradi wa maji wilayani Mbulu
………………………………………………………………..
Na Evaristy Masuha
Matumizi ya Utekelezaji Miradi ya maji kwa kuwatumia wataalamu wa wizara (Force account) mkoani Manyara umewezesha ongezeko la miradi tisa ambayo itasababisha wananchi 20,000 kufikiwa na huduma ya maji.
Akizungumza na wataalamu wa Wizara ya Maji walio katika ziara ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji mkoani humo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Manyara, mhandisi Walter Kirita amesema mpango ya awali ulikuwa ni kuwafikia wananchi 26,000. Hatahivyo baada ya kuanza kutekeleza miradi hiyo kwa kutumia mfumo huo wameweza kubakiza fedha ambazo zitapelekwa katika miradi mingine mipya.
“RUWASA makao makuu wamenunua vitu vingi kwa bei nzuri, tukaamua kutumia force account ambayo imewezesha kuongeza miradi mipya 9 ambayo itaongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi 20,000. Hii imekuwa zaidi ya matarajio kwani awali tulitarajia kwamba tungewafikia wananchi 26,000 pekee”, mhandisi Walter Kirita anabainisha.
Anasema kwa mwaka 2020/2021 RUWASA imetenga shillingi bilioni 13.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi 45 ambayo itasaidia upatikanaji wa maji kwa watu 157,903.
Ofisa na mtaalamu huyo wa maji amepongeza serikali kwa kuweka msisitizo katika utekelezaji wa miradi kwa kutumia force account kwani miradi mingi imeweza kukamilika kwa haraka na kwa gharama nafuu.
Amema wana uhakika wa kutekeleza miradi mingi zaidi kutokana na matokeo yaliyopatikana kutokana na matumizi ya mfumo huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Menejimenti ya Rasilimali watu kutoka Wizara ya Maji, Ingrid Sanda amewapongeza watumishi wa Wizara hiyo kwa kufanya kazi kwa bidiii.
Amesema Wizara inao wataalamu wakutosha hivyo matumizi ya force account ni nafasi nzuri ya kuonesha uwezo, ujuzi na maarifa waliyosomea.