************************
NA EMMANUL MBATILO
Wasambazaji wa bidhaa nchini wametakiwa kuzingatia taratibu za viwango ili walaji waweze kupata bidhaa ambayo ni bora na sahihi kwa matumizi.
Hivyo yeyote ambaye atabainika kuingiza bidhaa ambazo hazijakidhi ubora atachukuliwa hatua za kisheria.
Ameyasema hayo leo Mkaguzi Mwandamizi kutoka Shirika la Viwango Tanzania TBS, Mhandisi Donald Manyama baada ya Shirika hilo kufanya ukaguzi katika Supermarket kadhaa Jijini Dar es Salaam na kubaini baadhi ya bidhaa kutokidhi viwango.
Akizungumza baada zoezi hilo kumalizika Mhandisi Manyama amesema wamefanya ukaguzi na kubaini bidhaa hizo hazina muda wa kuzalishwa (Production date) na muda wa mwisho wa matumizi (Expire date).
Aidha Mhandisi Manyama amesema katika bidhaa ambazo wamezibaini hazijakidhi viwango bidhaa za vipodozi zimekutwa kwa wingi kuliko bidhaa nyingine.
“Bidhaa ambazo tumezibaini kuwa na makosa ni Shower gel,Shampoo,Conditioner na Hair food zote hazina muda wa kuzalishwa na muda wa mwisho wa matumizi yake”. Amesema Mhandisi Manyama.
Pamoja na hayo Mhandisi Manyama amesema kuwa bidhaa hizo ambazo wamezibaini kuwa na kasoro zinakadiriwa kuwa na thamani ya Shilingi Milioni 10.
Hata hivyo amesema kuwa upungufu wa uelewa kwa wauzaji wa bidhaa unasabibisha kuwepo kwa makosa hayo hivyo TBS itaendelea kuchukua hatua hatua hasa kutoa elimu kwa wale wote wanaoagiza bidhaa pia wataendelea kuwakumbusha wazalishaji wa bidhaa za ndani.