Na Mwandishi Wetu, BUKOBA
Mabingwa wa kihistoria timu ya Yanga SC wameng’ara ugenini baada ya kuwachapa wenyeji, Kagera Sugar kwa kuwachapa 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kiungo Mkabaji Serge Mukoko Tonombe aliwanyanyua mashabiki dakika za jioni akipachipa bao 73 baada ya kutuliza vizuri mpira kwenye boksi na kumchambua kipa Issa Chalamanda kwa shuti la juu kufuatia pasi ya mchezaji mwenzake wa zamani wa AS Vita Tuisila Kisinda.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inayofundishwa na kocha Mserbia, Zlatko Krmpotic inafikisha pointi saba baada ya mechi tatu, ikishinda mbili na sare moja katika mechi zake mbili za awali nyumbani, Dar es Salaam.
Mchezo uliotangulia leo mchana, Tanzania Prisons ilipata ushindi wa kwanza baada ya kuwachapa Namungo FC 1-0, bao pekee la Gasper Mwaipasi dakika ya 47 Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa.
Prisons wanafikisha pointi nne baada ya mechi tatu, kufuatia kufungwa na kutoa sare mechi mbili za awali ugenini, wakati Namungo FC, wawakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho msimu huu – wanabaki na pointi zao tatu kufuatia kufungwa mechi nyingine moja nyumbani na kushinda moja.