…………………………………………………………….
MJUMBE wa Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM amesema kati ya wagombea urais waliojitokeza, hakuna kiongozi zaidi ya Dkt. John Pombe Magufuli.
“Nimekuja kuomba kura kwa ajili ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi ili apate miaka mitano mingine kwa sababu hakuna kiongozi bora kati ya wote waliojitokeza zaidi ya Dkt. John Pombe Magufuli,” amesema.
“Wanaokuja kuomba uongozi ni wengi lakini hakuna chama chenye benki ya viongozi kama CCM. Hakikisheni mnatupatia viongozi wa CCM ili waweze kufanya kazi pamoja na kwa kuelewana.”
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Septemba 19, 2020) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa kijiji cha Butiama, wilayani Butiama, kata za Nyamuswa na Mugeta wilayani Bunda, akiwa njiani kuelekea Mugumu, Serengeti, mkoani Mara.
Ametumia mikutano hiyo kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Bunda, Bw. Boniface Chacha Getere, wagombea udiwani wa wilaya zote mbili za Butiama na Bunda. Mgombea ubunge wa jimbo la Butiama, Bw. Jumanne Sagini amepita bila kupingwa.
Amesema uongozi ni lazima utengeneze timu inayofahamiana na inayozungumza lugha moja. “Chama cha Mapinduzi kimeleta viongozi watatu safi. Kwa hiyo ukienda kupiga kura chagua hao watatu ambao ni mgombea urais, ubunge na udiwani.”
“CCM inaleta tochi inayowaka na kumulika maeneo ya kuleta maendeleo. Ili iwake na kuleta hayo maendeleo, naomba usichanganye betri kwa kuweka gunzi hapo katikati. Je, ukiweka gunzi, hiyo tochi itawaka na kumulikia maendeleo?”, alihoji na kujibiwa hapana.
Mapema leo, Mheshimiwa Majaliwa alipita nyumbani kwa Baba wa Taifa katika kijiji cha Mwitongo na kumjulia hali Mama Maria Nyerere.
Wakati huohuo, Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia wananchi hao kuwa Serikali ya awamu ya tano inajali matumizi ya fedha za umma na kwamba haina mchezo na wanaobainika kutumia vibaya fedha hizo.
“Fedha za umma zinazoletwa kwenye miradi ya maendeleo siyo za kugusa. Hakuna ufisadi, hakuna kula rushwa na watumishi wa umma wanajua kwamba ukizigusa tu, unaunguzwa mikono,” amesema.