*******************************
Na.Mwandishi Wetu
Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART unatarajia kuongeza na kuendeleza ushirikiano na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji NIT, ili kuboresha huduma za usafiri katika Jiji la Dar es Salaam hasa katika kipindi hiki ambacho Wakala unaendelea kutanua huduma zake katika njia mbalimbali kwaajili ya kuwapunguzia wananchi kero ya foleni na msongamano.
Akizungumza mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam katika Mahafali ya wanafunzi wa Lojistiki na Usafirishaji ,Mtendaji Mkuu wa DART Mhandisi Ronald Lwakatare amesema taaluma ya lojistiki na usafirishaji ni muhimu sana kwa mradi kama wa Mabasi Yaendayo Haraka kwani wataalam hao watasaidia kuboresha usafiri huo kutokana na tafiti mbalimbali watakazofanya kwaajili ya kuusaidia Wakala kuboresha huduma.
“Sisi kama Wakala tunathamini sana mchango wa wahitimu hawa kwasababu wanahitajika katika kufanya tafiti za kuboresha usafiri na usafirishaji mijini, mfano kwa sasa mradi wetu kuna shida kwenye maeneo ya vivuko vya watembea kwa miguu pengine tungedhani ni vyema vivuko hivyo vikawa chini ardhini na mabasi yakapita juu ama vikawa vya juu na mabasi yakapita chini, nyinyi ndio wakutushauri namna bora ya kutatua changamoto hii” Alisema Mhandisi Lwakatare.
Mhandisi Lwakatare alisema Jiji la Dar es Salaam linakua kwa kasi hivyo suala la usafiri wa umma wa uhakika na wa bei nafuu ni muhimu hivyo wanataaluma hao wana manufaa makubwa kwa Wakala na nchi kwa ujumla hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania imeingia kwenye uchumi wa kati hivyo shughuli za kila siku za wakazi wa Jiji zitaongezeka na watahitaji usafiri wa uhakika na wa kueleweka.
“Kwa kutambua umuhimu wa chama cha wanafunzi wa Lojistiki na Usafirishaji Wakala utawapatia Kompyuta moja pamoja na Printa ili muweze kuitumia katika kuimarisha shughuli zenu, hii pia itawawezesha kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitasaidia katika kuboresha huduma katika mradi wa BRT lakini pia katika sekta ya usafiri wa umma nchini Tanzania” Alisema Mhandisi Lwakatare.
Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi Meneja Leseni kutoka Mamlaka ya udhibiti wa Usafiri nchi kavu LATRA Bw.Leo Ngowi, amesema taasisi yake inatambua mchango wa wahitimu hao kwakuwa watasaidia kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya usafirishaji nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof. Zakaria Mganilwa amesema wataendelea kutoa wataalam katika Nyanja mbalimbali kwaajili ya kuisaidia nchi na katika soko la kimataifa.
Katika Mahafali hayo wahitimu 56 walitunukiwa vyeti katika Shahada ya Lojistiki na Usafirishaji.