Home Siasa MHE.DKT.MWINYI AAHIDI MAMBO MAKUBWA KWA WAJASIRIAMALI VISIWANI ZANZIBAR

MHE.DKT.MWINYI AAHIDI MAMBO MAKUBWA KWA WAJASIRIAMALI VISIWANI ZANZIBAR

0

MGOMBEA Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na makundi ya Wavuvi katika Kijiji cha Mpene Mwambe Wilaya Mkoani Pemba.

BAADHI ya Wananchi wa Kijiji cha Mpene Mwambe Wilaya ya Mkoani Pemba wakimsikiliza kwa makini Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Hussein Ali Mwinyi alipowatembelea leo kuomba ridhaa ya kuchaguliwa ifikapo Octoba 28,mwaka huu.

*************************************

NA IS-HAKA OMAR,PEMBA.

MGOMBEA Urais wa Zanzibar  kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais atawawezesha wajasiriamali kupata fursa za mikopo,mafunzo na masoko ili wajikwamue kiuchumi.

Alisema suala la ujasiriamali limepewa kipaumbele katika Sera za CCM hivyo kupitia  mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi watatoa mikopo yenye masharti nafuu ili iwasaidie wajasiriamali hao.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na makundi mbalimbali ya wajasiriamali katika mwendelezo wa ziara yake ya kukutana na wananchi huko katika Kijiji cha Michenzani Willaya ya Mkoani Pemba.

Dk.Hussein, alisema wajasiriamali wakiwezeshwa watapata fursa ya kutengeneza bidhaa zenye viwango zinazokubalika katika masoko ya kitaifa na kimaita.

Alisema katika serikali ijayo sekta ya ujasiriamali itapewa uzito wa kipekee kwani inawawezesha wanawake na vijana kujiajiri wenyewe.

“ Wanawake na vijana msiwe na hofu ujasiriamali ni sekta muhimu sana katika maendeleo ya nchi yetu hasa kwa wakati huu wa kuelekea katika uchumi mpya  kwa maslahi ya wananchi wote.“, alisema Dk.Hussein.

Katika maelezo yake Dk.,Mwinyi, alisema ataendeleza mazuri yaliyofanywa na Serikali inayomaliza muda wake sambamba na kubuni vyanzo vipya vya kiuchumi vitakavyoongeza pato la taifa na kuiwezesha serikali kutoa ajira nyingi kwa wananchi.

Alisema atatekeleza kwa vitendo vipaumbele vyake ambavyo ni kuimarisha huduma za kijamii zikiwemo kuboresha huduma za afya,elimu na upatikani wa huduma za maji safi na salama kwa wakati.

Alieleza kuwa ataimarisha sekta za miundombinu zikiwemo ujenzi na utanuzi wa barabara,kuimarisha miundombinu ya umeme na ujenzi wa bandari mpya zitakazotoa ajira kwa wingi.

Akizungumzia sekta ya uvuvi alisema atahakikisha wanapata vifaa vya kisasa vya uvuvi vitakavyowasaidia kuondokana na uvuvi wa zamani usiokuwa na tija.

“Nafahamu wavuvi na wakulima wa mwani mnakabiliwa na changamoto nyingi hasa ukosefu wa nyenzo za kisasa za uvuvi, nakuahidini nikipata kuwa Rais matatizo yayayowakabili nitayatatua.”, alifafabua Dk.Hussein.

Mapema akizungumza Katibu wa Jumuiya ya Wavuvi katika Kijiji cha Mwambe Mpene Wilaya Mkoani, Kheri Sheha Ali alisema wanakabiliwa na changamoto ya kutumia vifaa duni vya uvuvi hivyo wanaomba kupatiwa vifaa vya kisasa.

“Vyombo vyetu ni vya zamani kuna wakati baadhi ya wenzetu wanapoteza maisha kutokana na vifaa hivi hivyo tunaomba serikali itupatie boti za kisasa”, alisema Kheri.

Naye Mjasiriamali wa kijiji hicho Zaituni Sheha Faki, alisema akina mama wa kijiji hicho waliojiajiri wenyewe katika sekta ya ujasiriamali wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji hivyo alimuomba mgombea huyo pindi akiwa Rais atafute ufumbuzi wa changamoto hiyo.

Mgombea huyo wa Urais wa Zanzibar Dk.Hussein, aliwaombea kura wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi  za Marais hadi Madiwani  ili washinde katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Dk.Hussein amehitimisha ziara yake kisiwani Pemba na atarudi Unguja kuendelea na ratiba ya Kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoendelea nchini.