Mgombea wa Urais kupitia Tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia maelfu ya Wananchi wa Wilaya ya Chato katika mkutano wa Kampeni za Chama cha Mapinduzi CCM uliofanyika katika uwanja wa Mazaina Chato mkoani Geita.
(NA JOHN BUKUKU-CHATO GEITA)
Mgombea Urais kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. John Pombe Magufuli amesema Usalama wa nchi ni jambo muhimu sana kwa kila mtanzania na raia wote wa Tanzania na ni muhimu kuilinda kwa nguvu zote.
Amesema wakati wanaingia madarakani hali ya usalama wilayani Kibiti kulikuliwa na mauji na askari polisi 12 waliuawa kwa kupigwa risasi,hivyo walisimama imara kuimarisha ulinzi na usalama.
Rais Dk John Pombe Magufuli ameyasema hayo leo kwenye mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Mazaina mjini Chato mkoani Geita.
Rais Dk. Magufuli ametolea mfano nchi ya Rwanda ambayo iliwahi kukumbwa na mauaji ya Kimbari mwaka 1994 na kusababisha watu wengi kupoteza maisha ambapo amempongeza Rais wa Rwanda Mh. Paul Kagame kwa kurejesha amani ya nchi yake na kuhakikisha inakuwa salama mpaka sasa.
“Zamani ukitaka kusafiri lazima usindikizwe na Polisi nikasema hapana, majambazi hawawezi kutawala katika nchi hii, Hivyo navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusimamia hali ya ulinzi nchini kwetu,”amesema Dk.Magufuli na kuongeza nchi ikikosa usalama hakuna kinachoweza kufanyika.
Naye Katibu Mkuu wa CCM,Bashiru Ali Kakurwa amesema Chama hicho katika uchaguzi mkuu mwaka huu wamepanga kufanya mashambulizi katika awamu sita na tayari awamu ya kwanza imekamilika na sasa wameingia awamu ya pili.
”Nipo kukuombea kura wewe mwenyewe na wagombea wote wa CCM nchi nzima ili tuweze kuendelea kuongoza Taifa letu.
Tumemaliza awamu ya kwanza, na tutakuwa na raundi sita, raundi ya kwanza tayari na leo tunaanza raundi ya pili na kila raundi itakuwa nzito.Raundi ya pili itakuwa nzito kubwa kuliko raundi ya kwanza, na raundi ya tatu itakuwa nzito kuliko ya pili,”amesema Dk. Bashiru.
Dk Bashiru pia amemuomba mgombea Dk.Magufuli kuhakikisha anaendelea kushambulia kila kona kwani wapinzani wamejileta wenyewe, hivyo asiwaonee huruma.
Wakati huo huo alikanusha uvumi unaonezwa kwamba CCM inataka kushinda viti vingi katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu ili ibadili Katiba.
”Nataka kukanusha uvumi eti CCM inataka kushinda viti vingi, kwamba wakiwa wengi wanataka kubadilisha Katiba, nataka niseme iwe mwisho, hao ni watu waliochoka na kufirisika kisiasa . Dk.Magufuli anaomba miaka yake mitano ili amalize miaka 10,hata ongeza hata sekunde.
Mh. Rais nakukabidhi raundi ya pili usiwe na huruma wamejileta wenyewe, kulia na kushoto wewe nenda nao, wakienda nje wewe baki nchi endelea kuchapa kazi,”amemaliza Dk Bashiru.