……………………………………………………………………………..
Ikiwa Septemba 13 uzinduzi wa Kampeni katika Jimbo la Singida Mashariki,mgombea ubunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Miraji Mtaturu anaitumia siku ya Ijumaa kubadilishana mawazo na kuweka mikakati ya ushindi na makundi mbalimbali katika jamii.
Mtaturu amepata fursa ya kuzungumza na wazee kupitia vijiwe vyao vya kahawa na kupata busara zao Kama njia mojawapo ya kujipanga zaidi katika ushindi wa CCM.
Amesema wazee hao wanakijua Chama walichoishi nacho enzi na enzi,wanajua umuhimu wa CCM kwa Wananchi na kwa Taifa kwa ujumla na ndio maana Mara zote amekuwa karibu nao.
“Wazee wetu ni dawa,maneno yao na ushauri wao ukiutumia ni taa tosha ya kukupa mwanga katika safari yako hata patakapokuwa na giza utaweza fika,wazee hawa wanakijua Chama Chao tangu enzi za Hayati Mwalimu Julius Nyerere,hivyo baraka zao ni muhimu wakati wote,”alisema.
Mbali na wazee pia amekutana na wanamichezo wa timu ya Mawakala na Sokoni FC ambao katika kipindi Cha miezi tisa ya uongozi wake alizisadia timu hizo kupitia mashindano aliyoyapa jina la Elimu cup na kilimo mbunge Cup.
“CCM inagusa kila kona na ndio maana huwa inafananishwa na Maji kwamba usipoyanywa basi utayaoga,kupitia Ilani yetu iliyoisha na hii iliyopo Sasa inaeleza wazi namna itakavyoimarisha sekta ya michezo,nami nikiwa mmoja wa wasimamizi wa Ilani hiyo katika Jimbo langu nilijitahidi kuwa nao bega kwa bega wanamichezo,”alisema.
Akizungumzia kuhusu uzinduzi Mtaturu amesema unatarajiwa kufanyika siku ya jumapili katika viwanja vya stendi mpya Ikungi kuanzia saa sita mchana hadi saa 12 jioni.
“Viongozi mbalimbali wa Chama Mkoa watakuwepo,wanachama na wapenzi wa CCM,tutatumia mkutano huo kunadi Sera na Ilani yetu,sisi sio kama wengine wanaotumia majukwaa kuomba huruma ya wananchi,sisi tuna mengi ya kuwaeleza wananchi tuliyoyafanya na tunayotarajia kuyafanya mpaka muda unaonekana hautoshi,”alisema Mtaturu.
Uzinduzi huo utapambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii wakiongozwa na Mzee wa Bwax.