Jumuiya ya nchi za Afrika, Carribean na Pacific (OACPS) imetoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuondoa vizuizi vya kusafiri (travel
bans) kwa baadhi ya nchi za OACPS hususan zile zilizoonesha kuwa salama zaidi
dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Corona kama Tanzania. Wito huo ulitolewa
katika kikao maalum cha mashauriano baina ya Jumuiya ya nchi za OACPS na nchi
ya Ujerumani ambayo kwa sasa ni Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya. Mashauriano hayo yaliyofanyika tarehe 9 Septemba
2020 katika Ofisi za Jumuiya ya OACPS, Brussels nchini Ubelgiji, yaliongozwa na
Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa
Ulaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mabalozi wa nchi za OACPS walioko Brussels,
Mhe. Jestas Abuok Nyamanga na ujumbe wa Ujerumani uliongozwa na Waziri wa
Masuala ya Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo wa Serikali ya Shirikisho la
Ujerumani, Dkt. Gerd MÙLLER. Katika kikao hicho wajumbe walisisitiza umuhimu wa
Umoja wa Ulaya kuendelea kuunga mkono Shirika la Afya Duniani (WHO) katika
kusimamia ithibati za tafiti za chanjo za ugonjwa wa Corona na Shirika hilo
kuendelea kujengewa uwezo wa kusimamia utaratibu wa kuhakikisha kuwa chanjo
itakayothibitika inawafikia mataifa yote kwa usawa na kwa gharama nafuu. Kikao hicho kilijadili pia hatua mbalimbali
zinazopaswa kuongeza msukumo kwa Umoja wa Ulaya katika kuzisaidia nchi za OACPS
kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana na ugonjwa wa Corona hususan
katika sekta ya utalii na kilimo. Mikakati iliyojadiliwa ni pamoja na ile
inayolenga kupunguza, kufuta au kubadilisha masharti ya ulipaji wa madeni ya
nchi za Jumuiya ya OACPS na wito wa nchi za OACPS kuutaka Umoja wa Ulaya
kusogeza mbele utekelezaji wa baadhi ya kanuni na taratibu mpya za biashara
zilizopangwa kuanza kutumika mwanzoni mwa mwaka ujao ili kuzipa nafasi nchi za
OACPS kujipanga zaidi kabla ya kuanza kutumia kanuni hizo. Kupitia mashauriano hayo, pande zote mbili
zilitathmini mwenendo wa majadiliano ya Mkataba mpya wa ubia wa Ushirikiano wa
Kiuchumi baina ya nchi za Jumuiya ya OACPS na Umoja wa Ulaya yanayoendelea hivi
sasa baada ya mkataba wa sasa kufikia kikomo mwezi Desemba 2020. Pande mbili
zilijadili kwa kina namna ya kushirikiana katika maeneo yanayolenga kuongeza
mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo, uwiano ulio sawa katika biashara na
maendeleo ya teknolojia katika kukuza uchumi na maendeleo ya watu. Kikao kilihitimishwa kwa Ujerumani kuonesha utayari
wa kuyapa kipaumbele masuala yote yaliyojadiliwa katika kipindi cha uongozi
wake wa Baraza la Umoja wa Ulaya na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki katika kipindi hiki ambacho inashika nafasi ya Rais wa Baraza
la Mawaziri wa nchi 79 wanachama wa Jumuiya ya nchi za Afrika, Carribean na
Pacific itaendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya na kufanya kazi kwa karibu na
uongozi wa Ujerumani kwenye Baraza la Umoja huo wa Ulaya kusukuma ajenda zenye
manufaa na maslahi kwa pande zote mbili.
|