………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, DODOMA
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi(CCM), Anthony Mavunde ametoa ahadi saba kwa wananchi wa jimbo hilo ikiwemo kuchimba visima vikubwa vitano vya maji ili kuondoa kero ya maji kwa wananchi
Mavunde ametoa ahadi hizo leo katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika Kata ya Nala, Jijini hapa.
Amesema endapo wananchi wakimpa ridhaa tena ya kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo atahakikisha anatatua kero ya maji kupitia Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira(DUWASA) kwa kuchimba visima katika Kata ya Zuzu ili visambaze maji katika eneo la Nala,Mahungu,Zuzu na Nkuhungu.
Aidha, ameahidi ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Kata ya Nala ambapo tayari eneo la ekari 33 limetengwa.
“Miaka mitano mliyonipa ilikuwa ya kujifunza na nimeahidi na kutekeleza, naomba mnichague tena kukamilisha usambazaji wa umeme katika maeneo yaliyobakia kupitia Programu ya ujaziliaji(densification),”amesema.
Pia amesema atahakikisha anafungua barabara katika viwanja vipya vilivyopimwa.
Ameahidi kujenga shule za msingi mpya katika eneo la Segu na Nala.
“Pia nawaahidi nitashughulikia malipo ya fidia ya wananchi wanaopisha ujenzi wa barabara pete(ring road) na kushughulikia migogoro ya ardhi,” amesema