Home Mchanganyiko TEMESA YAKABIDHIWA VIFAA VYA KIUTENDAJI KATIKA KARAKANA

TEMESA YAKABIDHIWA VIFAA VYA KIUTENDAJI KATIKA KARAKANA

0

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akizungumza na uongozi  na wafanyakazi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), wakati wa uzinduzi wa vifaa stahiki vya karakana vitakavyosambazwa katika mikoa yote nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, pamoja na viongozi wengine wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa vifaa stahiki vya karakana vitakavyosambazwa katika mikoa yote nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Matengenezo na Huduma za Ufundi, Mhandisi Sylvester Semfukwe, akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, wakati wa uzinduzi wa vifaa stahiki vya karakana vitakavyosambazwa katika mikoa yote nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga, akitoa maelekezo kwa viongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), wakati akikagua baadhi ya vifaa stahiki vilivyonunuliwa kwa ajili ya karakana za Wakala huo katika mikoa yote nchini.

Baadhi ya vifaa stahiki vilivyonunuliwa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa ajili ya kuboresha na kuziongezea ufanisi katika utendaji kazi wa karakana na vitasambazwa katika mikoa yote nchini. Vifaa hivyo vimegharimu zaidi ya shilingi milioni 430.

…………………………………………………………………………………..

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imekabidhi kwa Wakala wa Ufundi na umeme (TEMESA) vifaa stahiki kwa ajili ya karakana za mikoa 14 na kituo kimoja (1) kikubwa vyenye gharama ya zaidi ya shilingi milioni 430 kwa lengo la kuboresha huduma za utengenezaji wa magari.

Vifaa hivyo  vitagawiwa katika katika mikoa/vituo vya wakala huo vilivyopo Dar es Salaam (Vingunguti), Mtwara, Mara, Simiyu, Kagera, Tabora, Iringa, Rukwa, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Songwe na Same.

Aidha, imeelezwa kuwa hii ni muendelezo wa awamu ya kwanza ya vitendea kazi vilivyosambazwa kwenye karakana za mikoa 12 na vituo viwili (2) vikubwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 na kuleta tija katika utoaji huduma bora kwa wateja na kuongeza mapato. 

Akizunguma wakati wa uzinduzi huo wa vifaa hivyo uliofanyika katika karakana ya MT. DEPOT jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, ameupongeza wakala huo kwa kuanza ukurasa mpya katika mikoa yote nchini ili kuondoa zile kero na malalamiko ya matengenezo ya magari yaliyokuwa yanatolewa dhidi yao.

“Kupokea vifaa ni jambo moja na kuvitumia, kuvitunza ni jambo lingine hivyo tumieni vifaa hivi kuleta tija na kuongeza ufanisi zaidi”, amesema Arch. Mwakalinga.

Mwakalinga, ameongeza kuwa Wizara ipo kwa ajili ya kuendelea kuiwezesha wakala kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa ufanisi na kasi zaidi ili kupunguza malalamiko ya wateja hususan katika matengenezo ya magari.

 

Awali akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Japhet Masele, amesema kuwa Wakala umeendelea kuzifanyia ukarabati karakana zake katika mikoa ya Dar es Salaam (Vingunguti), MT Depot, Dodoma, Singida, Mwanza na Mbeya katika mwaka wa fedha 2019/2020 na katika mwaka huu mpya wa fedha 2020/21 imeweka mpango wa ukarabati katika karakana za mikoa ya Mara, Tabora, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Kigoma, Arusha na Pwani.

Katika kuhakikisha huduma zinasogezwa karibu na mteja, Mhandisi Masele ameeleza kuwa Wakala umepanga kuanzisha karakana kwenye Wilaya zilizo umbali wa kilometa 120 kutoka katika karakana ya mkoa. 

“Wakala tayari umeshaanzisha karakana za Wilaya katika Wilaya za Kilombero na Kahama ambazo zinaendelea kutoa huduma na sasa tuko mbioni kuanza huduma katika karakana ngazi ya Wilaya katika mji wa Same Mkoani Kilimanjaro”, amefafanua Mhandisi Masele.

Mtendaji Mkuu Masele amemueleza pia Katibu Mkuu Mwakalinga kuwa Wakala unaendelea kukamilisha ukarabati wa miundombinu na majengo kwa ajili ya karakana ya Mkoa wa Songwe itakayoanza kazi rasmi mapema mwezi Septemba 2020.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ya Ushauri ya Wakala huo TEMESA, Prof. Idrissa Mshoro, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini TEMESA na kutoa fedha za kununua vitendea kazi vya kisasa kwa ajili ya karakana zote nchini na kuahidi na kuendelea kutoa ushauri stahiki katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoukabili wakala huo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano