Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango (kushoto) ambaye ni mgombea ubunge Jimbo la Buhigwe wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, akiwa katika matukio mbalimbali wakati wa uzinduzi wa kampeni katika Jimbo hilo uliofanyika kwenye Kijiji cha Mnanila Manyovu mpakani na nchi jirani ya Burundi. Uzinduzi huo pia ulihidhuriwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Mhandisi Atashasta Nditiye .
*************************************
Na Mwandishi wetu, Kigoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango ambaye ni mgombea ubunge Jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma ameahidi kuinua uchumi wa wananchi wa Jimbo hilo kwa kusimamia miradi itakayowezesha kuongeza kipato cha wananchi hao.
Dk. Mpango alitoa ahadi hizo katika Kijiji cha Mnanila, Manyovu wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, ambapo alisema kuwa miongoni mwa mambo atakayoyasimamia ni kuhakikisha zao la kahawa ambalo ndilo linalimwa kwa wingi na wananchi hao linaongeza kipato na kuleta maendeleo kwa wananchi wa Jimbo hilo.
Katika uzinduzi huo wa kampeni Dk. Mpango aliahidi kuwa katika kipindi cha miaka mitano atakayokuwa mbunge wa jimbo hilo Serikali itajenga Kituo Cha Forodha cha Pamoja katika eneo la Foronya na stendi kubwa ya mabasi katika Kijiji cha Mnanira Kata ya Manyovu, wilaya ya Buhigwe kilichopo mpakani na nchi ya Burundi.
Pamoja na hilo aliahidi kuwa Serikali itajenga shule maalum ya kidato cha tano na sita, utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji na kukamilisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ambao umeanza kutekelezwa kutoka Manyovu hadi Kasulu na kwamba atasimamia kwa karibu kuhakikisha miradi hiyo inakamilika.
akizungumza katika Mkutano huo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema kuwa Dk. Mpango ni hazina kubwa kwa wananchi wa Jimbo hilo na kuwaomba wananchi kumpa kura nyingi za ndiyo sambamba na kura za Mgombea wa Kiti cha Urais wa Chama Cha Mapinduzi Mh. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na madiwani.
Profesa Ndalichako alisema kuwa Dk. Mpango ameonyesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Buhigwe katika kusimamia maendeleo yao hivyo hawana budi kuhakikisha anashinda kwa kishindo
Naye Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Mhandisi Atashasta Nditiye alisema kuwa Dk. Mpango ni bingwa wa uchumi hivyo kwa wananchi wa Jimbo hilo kuwa naye karibu itawafanya kuwa na maendeleo ya haraka kutokana na mipango ambayo Mbunge huyo ataibua na kuiwekea mipango ya utekelezaji kwa kuitafutia fedha.
Nditiye alisema kuwa Dk. Mpango akiwa mbunge wa kuteuliwa na Rais alifanya mambo mengi ya jumla ikiwemo ujenzi wa barabara za kiwango cha lami kilometa 260 kutoka Manyovu wilaya ya Buhigwe hadi Kabingo wilaya ya Kakonko na kwamba pamoja na hayo akichaguliwa atafanya mambo mengi zaidi kwa ajili ya Jimbo hilo.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kirumbe Ng’enda alisema kuwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliiona rasilimali kubwa waliyonayo Waziri Mpango na Profesa Ndalichako ndiyo maana akawateua kuwa wabunge na baadaye kuwa Mawaziri hivyo itakuwa jambo la ajabu kama wananchi watashindwa kuona umuhimu wa wagombea hao na kushindwa kuwachagua.