Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Leskar Sipitieck (katikati) akiandika yanayozungumzwa kwenye kikao cha Alat cha mkoa huo, kilichofanyika mjini Babati, kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Joseph Guulo Mandoo.
Mwenyekiti wa Alat wa Mkoa wa Manyara, George Bajuta akizungumza wakati akifungua kikao cha Alat cha mkoa huo kilichofanyika mjini Babati
…………………………………………………….
MADIWANI wa Mkoa wa Manyara, wamesikitishwa na kitendo cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwahoji kila mara na kuagiza warudishe posho walizochukua jambo linalosababisha wavunjike moyo wa kufanya kazi zao.
Wakizungumza mjini Babati kwenye kikao cha jumuiya ya serikali za mitaa (Alat) cha mkoa huo, madiwani hao wameazimia kuonana na mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ili kuongelea jambo hilo.
Mwenyekiti wa Alat wa mkoa wa Manyara, George Bajuta alisema kitendo cha Takukuru kuwahoji madiwani na kuagiza warudishe posho walizochukua siyo sahihi kwani jambo hilo lingepaswa kuachwa.
Bajuta alisema kasoro zilizojitokeza kwenye baadhi ya halmashauri zisitumike kuwaadhibu madiwani wengine ambao hawastahili kwani hata posho zenyewe zinazotolewa kwao ni kidogo.
“Wabunge wanapatiwa mishahara mikubwa na posho nzuri sasa baadhi walipendekeza kuwa madiwani wanafuja fedha hivyo kusababisha hali hii ya udhalilishaji kujitoleza,” alisema.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Jackson Sipitieck alisema kuna haja ya mkuu wa mkoa huo, katibu tawala wa mkoa, kamanda wa Takukuru na mkuu wa usalama wa taifa wa mkoa, kukutana nao ili kujadili tatizo hilo.
Mjumbe wa Alat wa mkoa huo, Daines Peter alisema maslahi na haki ya madiwani ibaki palepale kwani wana majukumu mengi kwa ajili ya kutumikia wananchi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto, Lairumbe Mollel alisema maslahi ya madiwani ni madogo lakini wanajitolea ila suala hilo linawavunja moyo.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Nicodemus Tarmo alisema hata Rais John Magufuli aliwahi kusema kwenye kikao cha Alat Taifa kuwa posho za vikao wanazopokea madiwani kupitia utaratibu uliowekwa uachwe.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu vijijini, Joseph Mandoo alisema vikao vya madiwani vya vyama na vya kumchagua Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya wanapaswa kulipwa kwani ni maandalizi ya kikao cha baraza la madiwani.
Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbulu, Gidishanga alisema wabunge hawatetei tena maslahi ya madiwani ila mbunge wa jimbo la Chemba, Juma Nkamia amekuwa akiwasemea madiwani bungeni.
Katibu tawala msaidizi wa mkoa huo (serikali za mitaa) Kenedy Kaganda alisema kila diwani anapatiwa posho zake kulingana na stahili zake ikiwemo fedha za kujikimu.
Hata hivyo, kaimu mkuu wa Takukuru mkoani Manyara, Isdory Kyando alisema madiwani waliotakiwa kurudisha posho ni wale waliochukua miaka iliyopita na sasa bila kustahili kuzichukua.