Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (kulia) akiongea na viongozi wa kiwanda cha mbolea cha Minjingu cha Manyara leo alipowatembelea kukagua uzalishaji.Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Bw.Tosky Hans
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Minjingu cha Manyara Bw.Tosky Hans (kushoto) leo alipotembelea kukagua hali ya uzalishaji wa kiwanda hicho ikiwa ni mkakati wa wizara ya Kilimo kuhamasisha viwanda vya ndani kuzalisha mbolea bora na yenye gharama nafuu kwa mkulima.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha mbolea cha Minjingi Bw.Tosky Hans leo alipowasili kiwandani hapo mkoani Manyara kwa ziara ya kukagua hali ya uzalishaji mbolea.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa ameshika chupa ya mbolea ya maji (Booster) inayozalishwa na kiwanda cha Keen Feeders cha Arusha leo alipotembelea.Akiwa kiwandani hapo ameagiza bidhaa zote hizo zisajiliwe na kupata nembo ya ubora kabla hazijaingizwa sokoni ili kumlinda mkulima.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) Dkt. Stephano Ngailo (aliyesimama) akitoa maelezo kuhusu viwanda vya mbolea za maji leo katika kiwanda cha Keen Feeders Arusha.Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya alitembelea kiwanda hicho (katikati) na kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha Keen Feeders Bw.Alfred Massawe.Kiwanda hicho huzalisha lita 600,000 za mbolea maji (boosters) kwa mwaka.
………………………………………………………………………
Serikali imeviagiza viwanda vya mbolea nchini kuzalisha mbolea yenye viwango vya juu vya ubora na kuiuza kwa wakulima kwa gharama nafuu ili uzalishaji wa mazao uwe na tija na kuchangia ukuaji wa uchumi.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ametoa kauli hiyo leo mkoani Manyara alipotembelea kukagua kiwanda cha mbolea cha Minjingu.
Alisema ameamua kufanya ziara kwenye mikoa iliyo na viwanda vya mbolea ili kuona namna wanavyozalisha ili kukidhi upungufu mkubwa wa mbolea ndani ya nchi hali inayopelekea wakulima kununua kwa bei kubwa.
“ Nimeamua kufanya ziara hii kutembelea viwanda vya mbolea na kuongea na
wazalishaji ili kuhamasisha upatikanaji wa mbolea yenye virutubisho bora na itakayouzwa kwa bei nafuu kwa wakulima nchini” alisema Kusaya
Kusaya aliongeza kusema katika ziara zake nyingi mikoani alipokea malalamiko ya wakulima kuuziwa mbolea kwa bei kubwa na kutolea mfano mkoa wa Kagera
alikuta mfuko wa kilo hamsini wa DAP ukiuzwa kati ya shilingi 80,000 hadi 90,000 kutokana na mbolea hiyo kuagizwa nje ya nchi.
“ Lengo la serikali ni kumkomboa mkulima, lakini hatuwezi kufikia lengo hilo kama
mbolea itaendelea kuuzwa kwa bei kubwa nchini.Ndio maana Tunataka viwanda vijengwe hapa nchini “ Kusaya alisema.
Katibu Mkuu huyo alisema mahitaji ya mbolea nchini ni takribani tani 664,000 wakati uzalishaji kwenye viwanda vyote 12 umefikia tani 38,000 pekee kwa mwaka.
Akizungumza kuhusu changamoto za kiwanda cha mbolea Minjingu kuwa na
uzalishaji mdogo, Meneja Masoko wake Franks Kamhabwa alitaja tatizo la upatikanaji soko kukwamisha uzalishaji zaidi.
Kiwanda cha mbolea cha Minjingu kina uwezo wa kuzalisha tani 100,000 za
mbolea kwa mwaka kutokana na akiba ya madini ya Phosphate takribani tani milioni 8 hadi 10 kwenye mgodi wake lakini sasa hivi wanazalisha tani 23,598 kwa
mwaka.
Kamhabwa alitoa ombi kwa serikali kuwa kiwanda cha mbolea Minjingu kipewe
fursa ya kupata soko la ndani ya nchi kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Pamoja (BPS)
sawa na mbolea zinazoagizwa nje ya nchi .
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Minjingu Tosky Hans aliishukuru
serikali kwa kukiunga mkono kiwanda hicho hali inayojidhihirisha kupitia Viongozi
mbalimbali kuizungumzia vizuri mbolea ya Minjingu.
“ Kiwanda hiki kilikuwa yatima huko nyuma, tunashukuru serikali ya Awamu ya
Tano imetushika mkono kutusaidia bidhaa zetu sasa zinakubalika sokoni “ alisema
Hans
Hans alimweleza Katibu Mkuu huyo wa Kilimo kuwa malengo ya kiwanda cha
Minjingu ni kufikia uzalishaji wa tani 500,000 ifikapo mwaka 2025 na kuwa
wataanzisha mashamba ya majaribio ( Demo plots) katika halmashauri mbalimbali
ili zitumike kufundishia wakulima juu ubora wa mbolea ya Minjingu.
Katika hatua nyingine Kusaya alitembelea viwanda vya kuzalisha mbolea za maji (
Boosters) vya Kahela Feeders na Keen Feeders Ltd vya Arusha na kujionea hali ya uzalishaji bidhaa hiyo .
Akiwa katika kiwanda za mbolea Keen Feeders kilichopo Ngaramtoni Arusha
alifahamishwa kuwa kiwanda hicho huzalisha lita 600,000 za mbolea ya maji na
kuuzwa kwa wakulima hali inayosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao.
Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho cha Keen Feeders Alfred Masawe alisema
wanakutana na changamoto ya upatikanaji wa vifungashio na mitaji hali
inayopelekea bei ya mbolea hiyo kuwa juu .
Katibu Mkuu Kusaya akiwa kwenye viwanda hivyo alibaini kuwepo kwa
mapungufu ya bidhaa zinazozalishwa kutokuwa na nembo ya usajili wa ubora
kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kusaya ameagiza wamiliki wa viwanda vyote ambavyo havina usajili wa Shirika la Viwango (TBS) pamoja na mamlaka zingine za udhibiti kwenda kuomba leseni hizo ili wawe na uhakika wa soko na kulinda mazao ya wakulima na binadamu watakaotumia mazao yaliyozalishwa kwa mbolea hiyo aina ya Booster.
Kuhusu changamoto ya mitaji kwa wazalishaji wa mbolea za Booster ,Kusaya
amewataka waende Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) na Mfuko wa Pembejeo nchini ( AGTIF) kukopa kwa kuwa ni taasisi za serikali na zinatoa riba nafuu kwa wakulima na wananchi.
“Nendeni TADB na AGTIF kukopa mitaji ya kukuza uzalishaji wa mbolea kwenye
viwanda vyenu ili wakulima wapate mbolea hizo kwa gharama nafuu zaidi” alisema Kusaya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA)
Dkt.Stephano Ngailo aliyeambatana na Katibu Mkuu kwenye ziara hiyo amemshukuru kwa kazi kubwa aliyoifanya kutembelea na kuhamasisha wazalishaji mbolea kwenye mikoa mitano.
Dkt.Ngailo alisema amepokea malekezo yote ya serikali yaliyotolewa na Katibu Mkuu na kuwa watahakikisha wazalishaji wa mbolea nchini kote wanazingatia ubora na kuuza bidhaa hizo kwa gharama nafuu ili iwafikie wakulima wengi.
Kusaya pia ameagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) kufanya ukaguzi wa
mbolea zisizo na viwango (fake) ambazo zinalalamikiwa na wazalishaji wadogo kuwa zinaharibu soko lao kwa kuuzwa mitaani.
“ TFRA fuatilieni mbolea (booster) zisizo na ubora kwenye masoko ya Kariakoo, Arusha, na kwingineko mikoani na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wauzaji na watengenezaji ili kudhibiti zisiendelee kusambaa.Nipate taarifa yenu ya utekelezaji mapema.” aliagiza Katibu Mkuu Kusaya akiwa Arusha.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo amehitimisha ziara yake ya kutembelea viwanda vya mbolea na kukutana na wazalishaji katika mikoa ya Dar es Salaam,Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambapo imemwezesha kujionea hali halisi ya uzalishaji na upatikanaji mbolea nchini.