****************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewatakaviongozi wote na watendaji wa Serikali kuanzia ngazi ya kijiji, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi wizara kuwajibika ipasavyo na kudumisha nidahmu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Amesema ili kufikia lengo na dhamira ya kutekeleza Mpango na Bajeti ya Serikali ya 2019/2020 kwa ufanisi, viongozi hao wanatakiwa waendelee kuwasisitiza wananchi washiriki ipasavyo kulinda miundombinu inayojengwa kwa gharama kubwa na Serikali.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 28) wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Septemba tatu mwaka huu.
Pia, Waziri Mkuu amezitaka mamlaka husika zishirikiane na wadau wengine katika kudhibiti uharibifu wa mazingira kwa kukomesha ukataji hovyo wa misitu, uchafuzi wa bahari, mito na maziwa na taka za plastiki ili kulinda mazingira asilia.
Akizungumzia kuhusu bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Waziri Mkuu amesema Serikali imepanga kutumia jumla ya sh. trilioni 33.11, kati yake sh. trilioni 20.86 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63. “Aidha, sh. trilioni 12.25, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania pamoja na Washirika wa Maendeleo waiunge mkono Serikali katika kutekeleza vipaumbele vilivyowekwa kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 ili viweze kutoa mchango wa haraka katika maendeleo ya uchumi na ya watu.
Wakati huo huo,Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu uboreshwaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, ambapo amesema kwa sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakamilisha maandalizi hayo ikiwa sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.
“Uboreshaji huo, unatarajiwa kuanza tarehe 18 Julai, 2019 katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambapo litafanyika kwa muda wa siku 7 kwa kila kituo na kuendelea hadi tarehe 5 Machi, 2020 litakapohitimishwa katika mkoa wa Dar es Salaam.”
Waziri Mkuu amesema uboreshaji huo hautahusisha wapiga kura walioandikishwa mwaka 2015 isipokuwa utawahusu wapiga kura wapya waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea au watakaotimiza umri huo ifikapo siku ya uchaguzi mkuu ujao.
Ametaja kundi lingine litakalohusika na zoezi hilo kuwa ni pamoja na wale watakaoboresha taarifa zao, kama waliohama jimbo au kata na kuhamia katika maeneo mengine ya kiuchaguzi, waliopoteza au kadi zao kuharibika, watakaorekebisha taarifa zao pamoja na kuwaondoa waliopoteza sifa kama vile kufariki.
Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kutumia fursa hiyo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura ili kutimiza haki yao ya kikatiba.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa Novemba mwaka huu kutakuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambao ni sehemu muhimu katika kuimarisha utawala bora na demokrasia ambayo imeendelea kunawiri nchini. Amewataka wananchi wenye sifa kujitokeza wakati utakapofika.
Amesema Serikali imeendelea kutumia mbio za mwenge kuhamasisha wananchi washiriki uchaguzi huo kupitia kaulimbiu isemayo “Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”.
“Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla hususan wale wenye sifa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kupiga kura ili waweze kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua au kuchaguliwa katika uchaguzi huo.”
Kwa wananchi wenye nia ya kugombea katika uchaguzi huo, Waziri Mkuu amesema ni lazima wajue majukumu wanayoomba kwamba yanahitaji umakini mkubwa na uchapaji kazi kwa sababu Serikali imewekeza miradi mingi kote nchini, hivyo wanahitajika watu walio tayari kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo ili itoe matokeo yanayokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuhakikisha uwepo wa mazingira salama na tulivu kwa kipindi chote cha uchaguzi.