Mkuu  wa   wilaya ya Iringa  Richard Kasesela wa pili  kushoto  akiwa na  diwani wa Mwangata Nguvu  Chengula (mwenye  suti  nyeusi) na  viongozi  wengine  wakimtazama mama wa watoto  watatu  ambao nusuru  wapoteze maisha kwa  kukosa huduma ya matibabu

***********************
Na Francis Godwin, Iringa
Serikali ya  wilaya ya  Iringa imepongeza   jitihada  za   diwani  wa kata ya Mwangata Nguvu  Chengula (CCM)  za  kuokoa maisha ya  mkazi wa Mwangata D Amida Mgonakulima  na wanae  watatu  wasife  kwa kukosa matibabu  baada ya  kutelekezwa na ndugu wakiwa  nyumbani.

Pongezi  hizo  zimetolewa na  mkuu  wa  wilaya ya Iringa Richard kasesela  leo  baada ya  kuwatembelea  wagonjwa  hao  waliolazwa katika  Hospitali ya Rufaa ya  mkoa wa Iringa    wakiendelea na matibabu ,kuwa  jitihada   hizo  zilizochukuliwa  na diwani  huyo ni  za  kupongezwa  kwani bila  kufanya  hivyo  uwezekano  wa mwanamke  huyo na  wanae  kupona  ulikuwa ni mdogo.

“Nimefarijika  sana  kuona  hali  ya  wagonjwa hao  ikiendelea  vizuri maana  huyo  mama  wa  watoto  alianza  kuoza kuanzia  kiunoni  kushuka  chini na  hakuwa na uwezo  hata  wa  kusimama  kitandani lakini kwa  sasa  afya  yake  inazidi  kwenda  vizuri   hakika  diwani  Chengula  kanusuru uhai  wao “ alisema Kasesela .

 Huku akitoa  agizo kwa  viongozi  wa  serikali za  mitaa katika wilaya  ya Iringa  kufanya msako  nyumba kwa  nyumba  ili  kujua watoto  ama  wagonjwa  waliotelekezwa  kwa  kukosa  huduma za matibabu.

“ Yawezekana kabisa  wagonjwa hao ni baadhi tu ya  wagonjwa  wengi  ambao  wamefungiwa  ndani bila  kutibiwa  sasa  naagiza  watendaji wa mitaa kupita  nyumba kwa nyumba  kukagua  na kama  kuna nyumba mlango  utakutwa  umefungwa  fungueni kagueni  ndani mkiwa na mwenye  nyumba  ili kujua ndani kuna  nini “ alisema Kasesela

Kasesela  alisema  tukio  jingine kama  hilo la Mwangata la mgonjwa  kutelekezwa  amelisikia kijiji cha  Kisanga na amekwisha  tuma  watendaji  kwenda  kufuatilia  na  kuwa matukio yote hayo ni ya  kikatili na hatakubali  kuyasikia ama  kuyaona ndani ya wilaya yake.

Kwa upande wake  diwani Chengula  alisema uamuzi wa   kunusuru  uhai wa wagonjwa hao ulikuja baada ya  wananchi  wake  kutoa taarifa  na kuwa ataendelea  kuwasaidia wagonjwa hao hadi watakapopona  .

Aidha Chengula ambae  leo  ameweza  kuungana na mkuu  huyo wa wilaya ya Iringa  kukabidhi mahitaji mbali mbali zikiwemo  nguo  na mengine  amejitolea  kumsomesha  motto  wa darasa la tatu katika  shule  yake ya  Sun Academy  ambapo  ada  yake  kwa mwaka ni  zaidi ya shilingi milioni moja na kuwa atamlipia kwa  miaka  yote na  kumwendeleza  .